IQNA

Uwanachama wa Mashia katika Baraza la Maulamaa wa Saudi Arabia

18:36 - February 17, 2009
Habari ID: 1745363
Kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Mfalme Abdallah bin Abdul Aziz wa Saudi Arabia katika muundo wa Baraza la Maulamaa la nchi hiyo, wataalamu wa mambo wanaelezea kuwepo uwezekano wa kujumuishwa wanafikra wa Kishia wa nchi hiyo katika baraza hilo.
Kanali ya habari ya Raswid imeripoti kuwa, licha ya kuwa hivi sasa ni wanazuoni wa madhehebu ya Hanbal tu ndio walioko katika baraza hilo, lakini wanazuoni wa madhehebu yote ya Sunni na vilevile Shia wanatazamiwa kujumuishwa katika baraza hilo kwa mara ya kwanza kufuatia mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Mfalme Abdallah katika baraza hilo.
Abdul Aziz al-Wahbi, mchambuzi wa mambo wa Saudi Arabia amesema kwamba, kuwekwa kwa maulamaa wa Kishia katika baraza lililotajwa kutatatua matatizo mengi ya kimadhehebu na kiutamaduni yanayoikabili jamii ya nchi hiyo hivi sasa. Ameongeza kuwa, mabadiliko ambayo yamefanywa katika baraza hilo yatapelekea kuongezwa kwa wanachama wa baraza hilo na hivyo kuwepo kwa mchanganyiko wa maoni na fikra tofauti kwa manufaa ya taifa la Saudi Arabia na umma mzima wa Kiislamu.
Jumamosi iliyopita, Mfalme Abdallah alichukua hatua isiyo ya kawaida katika kipindi cha utawala wake wa miaka mitatu iliyopita, ya kufanya marekebisho makubwa katika vyombo muhimu vya utawala wa nchi hiyo, zikiwemo wizara, tasisi za kiuchumi na kisheria.
Baraza la Maulamaa, Baraza Kuu la Sheria, Taasisi ya Kuamrisha Mema na Kukataza Mabaya na jumuiya za haki za binadamu ni miongoni mwa taasisi muhimu za nchi hiyo zilizofanyiwa marekebisho hayo makubwa. Mabadiliko hayo yamempelekea mwanamke kuteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Malezi. 365315
captcha