IQNA

Kanisa la Makopti wa Misri lalaani dharau dhidi ya Nabii Issa (as)

10:23 - February 21, 2009
Habari ID: 1746466
Kanisa la Makopti wa Misri limetoa taarifa likilaani vikali dharau iliyofanywa hivi karibuni na televisheni moja ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Nabii Issa na mama yake mtakatifu Maryam (as).
Kwa mujibu wa gazeti la Saudi Arabia la al-Watan, kanisa hilo limesema kuwa kitendo hicho cha Wazayuni ni dharau ya wazi kwa Nabii Issa Masih (as) pamoja na mama yake mtakatifu na kwamba ni matusi kwa matukufu ya kidini, jambo linaloonyesha kutokuwa na haya utawala ghasibu wa Israel.
Swalib Matta Sawires, mwanachama wa Baraza la Kieneo la Makopti wa Misri amesema kuhusiana na suala hilo kwamba, si jambo la kushangaza kwa Wazayuni ambao wameghusubu ardhi za Wapalestina na kutumia silaha zilizopigwa marufuku dhidi ya wanawake na watoto wao pamoja na kukanyaga haki za kimsingi kabisa za binadamu katika ardhi hizo, kufanya kitendo kama hicho cha dharau dhidi ya matukufu ya kidini. Ameendelea kusema kuwa, Waisraili wanadhani kwamba wao ni jamii teuliwa na iliyo bora zaidi kuliko jamii nyinginezo ulimwenguni na kwamba hiyo ni moja ya sababu zinazowapelekea kukanyaga itikadi na matukufu ya wenzao bila kujali lolote.
Mwanachama huyo wa Kanisa la Makopti wa Misri amemaliza kwa kusisitiza kwamba, jamii ya kimatifa inapasa kuchukua hatua za dharura kwa lengo la kuuzuia utawala huo kuendelea kufanya dharau dhidi ya dini. Amesema, watenda vitendo kama hivyo vya dharau wataendelea kuvikariri hadi siku ya Kiama na kwamba majina yao yatasajiliwa katika historia kuwa wahalifu.
Siku chache zilizopita kanali ya kumi ya televisheni ya utawala ghasibu wa Israel ilidai kuwa, mama yake Nabii Issa Bibi Maryam (as) hakuwa bikira kama wanavyosema Wakristo na Waislamu. Mwendeshaji wa kipindi cha televisheni hiyo pia alikebehi na kuchezea shere miujiza na Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu. 366803
captcha