Taarifa ya Umoja wa Ulaya imeutahadharisha utawala ghasibu wa Israel ikiutaka kutazama upya mipango yake ya ujenzi wa vitongoji zaidi vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.
Taarifa hiyo imesema kuwa hatua hiyo ya Israel ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, uvamizi wa ardhi za Palestina na ukiukaji wa ahadi za Israel kwa Palestina na jamii ya kimataifa.
Imesema kuwa ujenzi wa vitongo vya walowezi katika ardhi za Palestina unakwamisha juhudi za kurejesha amani Mashariki ya Kati na kuharibu jitihada zote za jamii ya kimataifa za kuimarisha amani ya kudumu katika eneo hilo.
Umoja wa Ulaya umesisitiza katika taarifa hiyo kwamba juhudi za kurejesha amani Mashariki ya Kati hazitakuwa na faida yoyote maadamu ardhi ya Palestina inaendelea kuvamiwa.
Mwaka uliopita Israel ilipanua zaidi mipango yake ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa kujenga nyumba 1200 katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina. 367221