IQNA

Mashindano ya Qur'ani na Hadithi yapewe umuhimu na vyombo vya habari

14:15 - February 24, 2009
Habari ID: 1748194
Naibu Mwenyekiti wa Kitengo cha Utamaduni na Malezi cha Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Jamiatul Mustafa nchini Iran ametoa wito kwa vyombo vya habari kuakisi ipasavyo mashindano ya kila baada ya miaka minne (olimpiadi) ya kimataifa ya Qur'ani na Hadithi akisisitiza kuwa mashindano hayo yanapaswa kupewa umuhimu katika vyombo vya habari.
Hujjatul Islam Walmuslimi Nasrullah Pejmanfar amesema kuwa vyombo vya habari vinapaswa kufanya juhudi kubwa za kutangaza mashindano ya kimataifa ya olimpiadi ya Qurani na Hadithi ili kuvutia idadi kubwa ya watu na kuzidisha taathira ya mashindano hayo. Sheikh Pejmanfar amesema, inasikitisha kwamba licha ya mashindano hayo yanayofanyika nchini Iran kushirikisha Waislamu kutoka nchi mbalimbali duniani, lakini hayakupewa umuhimu unaostahiki katika vyombo vya habari.
Sheikh Nasrullah Pejmanfar amesema kuwa Qur'ani Tukufu ni tiba ya matatizo yote ya maisha ya mwanadamu na akaongeza kuwa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani na Hadithi yanatayarisha uwanja mzuri wa kueneza mafundisho ya Qur'ani katika maisha ya mwanadamu.
Nasrullah Pejmanfar amesema kuwa harakati za Qur'ani zinazofanyika katika maeneo mbalimbali duniani zimekuwa zikijihusisha zaidi na suala la kuhifadhi kitabu hicho bila ya kutilia maana zaidi maarifa na ujumbe wa Qur'ani. Kwa msingi huo amesisitiza juu ya udharura wa kupewa umuhimu kadhia ya maarifa na maana ya aya za Qur'ani katika mashindano ya kimataifa.
Amesema kuwa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani na Hadithi nchini Iran yatazihamasisha nchi mbalimbali za Kiislamu kutilia maanani umuhimu wa maarifa na maana ya Qur'ani na kwamba mashindano hayo ni fahari kubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 367968
captcha