IQNA

Mashindano ya kitaifa ya Qur’ani yaanza kusini mwa Iran

10:18 - February 28, 2009
Habari ID: 1749230
Mashindano ya kitaifa ya Qur’ani yanayosimamiwa na Jumuiya ya Waqfu na Masuala ya Kheri yalianza jana katika mji wa Bushehr kusini mwa Iran.
Awamu ya sasa ya mashindano hayo inawahusisha wanaume peke yao. Sherehe za ufunguzi wa mashindano hayo zilihutubiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Swadiq Mahsuli ambaye amesema kuwa Qur’ani Tukufu ndicho kitabu chenye itibari zaidi cha Mwenyezi Mungu na kitabu pekee kilichosalimika na upotoshaji wa mwanadamu. Amesema kuwa Qur’ani ni hakika iliyoteremshwa kutoka kwa Mola Muumba ikibainisha mema na mabaya na kwamba Waislamu walifikia ustaarabu mkubwa kwa kushikamana na mafundisho ya kitabu hicho.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema kuwa suala la kusimamisha uadilifu na kujenga uhusiano wa karibu kati ya mwanadamu na Mola Muumba ni miongoni mwa malengo makuu ya Qur’ani Tukufu.
Naibu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waqfu na Masuala ya Kheri ya Iran Hujjatul Islam Walmuslimin Ahmadiyan amehutubia pia kikao cha ufunguzi wa mashindano hayo akieleza harakati kubwa zilizofanyika nchini katika medani ya kueneza maarifa ya Qur’ani Tukufu. Amesema kuwa jumuiya hiyo inatoa kipaumbele zaidi kwa suala la tafsiri ya Qur’ani na kwamba kwa sasa inasimamia darsa 1200 za tafsiri ya Qur’ani kote nchini.
Sheikh Ahmadiyan amesema kuwa katika kipindi cha kwanza cha mwaka huu wa Kiirani, taasisi hiyo imechapisha zaidi ya nakala laki nne za Qur’ani ili kukidhi mahitahi ya wasomaji wa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Nakala hizo zimetawanywa bure katika vituo na vyuo vya Qur’ani.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa zaidi ya watu elfu 30 walishiriki katika mashindano ya awali ya Qur’ani Tukufu hapa nchini. Washindi katika mashindano hayo ya awali wanachuana katika awamu ya sasa ya mwisho ya mashindano hayo. 369959
captcha