Ayatullah Hashimi Rafsanjani ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa Iraq Adil Abdulmahdi mjini Baghdad. Sheikh Rafsanjani amesema kuwa lengo la safari yake nchini Iraq ni kujadili jinsi ya kuhamisha uzoefu wa Iran kwa Waislamu wa Iraq kuhusu ujenzi mpya wa nchi hiyo na kukutana na maulamaa, wasomi na viongozi wa serikali ya Iraq kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili.
Ayatullah Rafsanjani amewapongeza wananchi wa Iraq kwa uvumilivu na subira yao kubwa katika kukabiliana na mashaka ya aina mbalimbali na akongeza kuwa Wairaq ni watu wenye historia adhimu duniani na waostahiki kuwa na maisha bora ya ustawi na maendeleo.
Amesisitiza juu ya kufanyika juhudi za kuijenga upya Iraq na akasema, Iran ya Kiislamu iko tayari kutoa uzoefu wake kwa Iraq katika nyanja za uchumi, viwanda, biashara na utamaduni.
Ayatullah Hashimi Rafsanjani amesisitiza juu ya udharura kuwepo mshikamano na umoja kati ya kaumu, madhebu na makundi mbalimbali ya Iraq.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Iraq amesisitiza juu ya kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande mbili na akasema kuwa Tehran na Baghdad zina uwezo mkubwa katika nyanja mbalimbali ambao unaweza kusaidia juhudi za ustawi katika nchi hizo mbili. Vilevile ameishukuru serikali na taifa la Iran kwa msaada wake katika kuimarisha usalama na amani nchini Iraq. 371403