Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Tehran imesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa kutegemea ibara ya pili ya hati ya Interpol na makubaliano ya Geneva ya mwaka 1949 yanayoitaka Polisi ya Kimataifa kuwalinda raia. Imesema kuwa ombi la kutiwa nguvuni watenda jinai za kivita wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza limetolewa baada ya uchunguzi wa faili hilo. Imesisitiza kwamba uchunguzi kuhusu watu wengine zaidi ya mia moja waliohusika na jinai za vita huko Gaza bado unaendelea.
Maelezo kuhusu watuhumiwa hao yameambatanishwa na picha zao. Orodha ya watenda jinai za kivita wa Israel katika Ukanda wa Gaza inajumuisha Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert, Waziri wa Mambo ya Nje Tzipi Livni na Waziri wa Vita wa utawala ghasibu wa Israel Ehud Barak. Kibali cha kutaka kutiwa nguvuni watenda jinai hao kimewasilishwa katika nchi 180 kote duniani.
Tarehe 27 Disemba mwaka jana jeshi la utawala ghasibu wa Israel lilianzisha mashambulizi makali ya anga dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza baada ya kulizingira eneo hilo kwa muda mrefu. Hujuma hiyo ilifuatiwa na mashambulizi ya nchi kavu ambayo yalipelekea kuuawa zaidi ya Wapalestina 1300 wakiwemo wanawake 111 na watoto wadogo 281. Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel pia liliharibu nyumba 2400, shule 29, vituo 30 vya kidini na maelfu ya mashamba ya Wapalestina. 371404