Ustadh Mustafa Ismail, alikuwa ni shule nzima ya usomaji Qur'ani ambapo wasomaji wa Misri na ulimwengu mzima wa Kiislamu walinufaika nayo. Aliwaachia wasomaji Qur'ani na Waislamu wote kwa ujumla, usomaji wa kuvutia wa kitabu hicho kitakatifu, ambao haufungamani na wakati wala zama.
Mustafa Ismail alizaliwa katika kijiji cha Tanta nchini Misri. Alipata elimu yake ya msingi chini ya usimamizi wa Ustadh Sayyid al-Badawi na kisha akaelekea katika Taasisi ya al-Ahmad katika eneo hilohilo la Tanta kwa madhumuni ya kuendelea na masomo yake huku akiandamana na Ustadh Mahmoud Khalil al-Hasri. Wakiwa huko, walishughulika na masomo yao ya juu ya Qur'ani chini ya Ustadh Ibrahim Salam, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi mashuhuri wa Misri katika zama hizo.
Akielezea sifa maalumu za Mustafa Ismail, Abdul Fatah Ali at-Taruti, mmoja wa wasomaji mashuhuri wa Qur'ani nchini Misri anasema katika mahojiano yake na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa IQNA kuwa, Marehemu Mustafa Ismail alikuwa na mbinu na lahani maalumu ya usomaji Qur'ani jambo lililowavutia sana wasikilizaji wake, na kuwafanya wasikilize usomaji wake wa Qur'ani kwa masaa bila kuhisi uchofu.
at-Taruti amesema, Mustafa Ismail alikuwa akizingatia vyema maana ya aya alizokuwa akizisoma na kuziakisi vizuri katika lahani yake ya usomaji, jambo lililotoa mvuto maalumu kwa wasikilizaji wake na hivyo kuwaathiri sana. 373680