Hassan Shaghlomi, Mkuu wa Baraza la Waislamu wa mji mdogo wa Darzi ulioko kaskazini mwa mji mkuu wa Ufaransa Paris, amesema wakati wa kufanyika kikao cha pamoja cha Baraza la Mayahudi la Val-de-Marne kwamba, hivi karibuni Waislamu wa nchi hiyo watabuni Jumuiya ya Maimamu wa Swala za Jamaa.
Amesema lengo kuu la jumuiya hiyo litakuwa ni kuimarisha mawasiliano kati ya maimamu wa swala za jamaa wa miji mbalimbali ya nchi hiyo na kuwasilisha matatizo ya Waislamu kwa viongozi husika wa serikali.
Akibainisha nafasi muhimu ya maimamu katika jamii ya Ufaransa, Shaghlomi amesisitiza kwamba mamimamu hubeba na kueneza ujumbe muhimu wa amani na suluhu wa dini tukufu ya Kiislamu. Huku akibainisha msimamo usio wa kisiasa wa jumuiya hiyo, Rashid Meimuni, mmoja wa waanzilishi wa jumuiya hiyo amesema kuwa, kinyume na jumuiya nyinginezo za Kiislamu, jumuiya hiyo haina nia ya kujihusisha na masuala ya kisiasa.
Andre Benayoun, mkuu wa baraza lililotajwa la Mayahudi amesema kuwa kushiriki kwa idadi kubwa ya makundi tofauti ya kidini katika kikao kilichomalizika hivi karibuni cha Ufaransa Baada ya Gaza ni ishara ya wazi inayothibitisha kwamba raia wasio wa Kikristo wa nchi hiyo wanaipenda sana nchi yao. Amesema, hivi karibuni anapanga kufanya safari ya kuzitembelea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni huku akiwa ameandamana na makundi mbalimbali ya kidini ya vijana wa Ufaransa. 377421