IQNA

Waislamu wautaka Umoja wa Mataifa uzuie kutusiwa dini

11:40 - March 14, 2009
Habari ID: 1755619
Nchi za Kiislamu zimeliandikia barua Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zikilitaka lipasishe azimio la kupiga marufuku kutusiwa matukufu ya kidini.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, huku ikikosoa kuongezeka kwa vitendo vya dharau na matusi dhidi ya dini za mbinguni katika nchi za Magharibi, Pakistan ameliandika baraua baraza hilo kwa niaba ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, ikisema kuwa jambo hilo ni ishara ya wazi ya kuongezeka vitendo vya utumiaji nguvu wa kidini duniani.
Pakistan pia imeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na kuongezeka vitendo vya chuki na uchochezi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi na kukosoa vikali kuhusishwa ugaidi na dini hii tukufu yenye kuhimiza amani duniani kufuatia mashambulio ya Septemba 11.
Imeashiria kuchapishwa kwa vikaragosi vya matusi dhidi ya Mtume Muhammad (saw) katika magazeti ya Denmark na kusisitiza kwamba, kupotoshwa kwa sura na mafundisho halisi ya dini mbalimbali kupitia vyombo vya habari kunapotosha fikra za waliowengi duniani kuhusiana na dini hizo na hivyo kupelekea baadhi ya watu kutusi bila kusita matukufu ya dini ya Kiislamu. Barua hiyo itachunguzwa katika kikao kijacho cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Kama kawaida yazo, nchi nyingi za Magharibi zimepinga vikali kuwasilishwa na kujadiliwa kwa suala hilo katika baraza hilo la haki za binadamu. 377432
captcha