IQNA

Utambulisho wa Kiislamu kuthibiti ulimwenguni kupitia umoja wa Kiislamu

15:54 - March 17, 2009
Habari ID: 1756739
Haja ya kuwepo umoja, mfungamano na mshikamano inahisika zaidi miongoni mwa Waislamu kuliko mataifa mengine yote, na utambulisho wa Waislamu unaweza tu kuthibitishwa mbele ya walimwengu kupitia umoja wa mwisho wa Kiislamu.
Hayo yamesemwa na Burhanuddin Rabbani, Rais wa zamani wa Afghanistan ambaye alikuwa akizungumza hivi karibuni pambizoni mwa kikao cha kimataifa cha 22 cha Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran. Amesema pamoja na kuwepo matatizo mengi nchini Afghanistan, lakini Waislamu wa nchi hiyo wanaendelea mbele na maisha yao ya kawaida na kwamba wamepata mafanikio makubwa ya kisiasa na yasiyo ya kisiasa katika miaka ya hivi karibuni. Amesema, hii leo kuna ushirikiano na umoja wa kupigiwa mfano miongoni mwa Masuni na Mashia wa Afghanistan licha ya kuwepo njama kubwa za kuwatenganisha wafuasi wa madhehebu mbili hizi muhimu za Kiislamu.
Rais wa zamani wa Afghanistan amesema, hitilafu za kihistoria zimewasababishia Waislamu matatizo mengi na kuwafanya wapoteze nafasi yao muhimu katika ngazi za kimataifa. Amebainisha masikitiko yake makubwa kuhusiana na Waislamu kutoweza kufikia maendeleo katika nyanja mbalimbali za maisha na kusema kuwa, kazi yao imekuwa ni kuiga maendeleo ya wangine jambo ambalo limekuwa likizusha hitilafu na migongano miongoni mwao.
Amesema, wasomi wa zama hizi kama Sayyid Jamaludeen Asadabadi na Imam Khomeini (MA), mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran walitoa mchango mkubwa katika kuunganisha umma wa Kiislamu na kuongeza kwamba Waislamu wanapasa kufanya juhudi maradufu ili kuimarisha umoja na mshikamano kati yao. 378466
captcha