Kikao cha falsafa na irfani ya Kiislamu ambacho kimeandaliwa na kundi la utafiti wa Kiislamu la Kituo cha Utafiti wa Utamaduni cha Kimataifa cha Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu nchini Iran kimefanyika nchini Bulgaria kwa ushirikiano wa Kitengo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kikoa hicho kimehudhuriwa na wanafikra wa Bulgaria pamoja na wasomi wa Kiirani. Wazungumzaji wa kikao hicho wamesisitiza juu ya umuhimu wa falsafa na irfani ya Kiislamu katika maisha ya mwanadamu na kugusia baadhi ya tofauti zilizopo kati ya elimu mbili hizo muhimu na elimu kama hizo zinazofundishwa katika maeneo mengine ya dunia.
Wamesema, lengo muhimu la elimu ya irfani ya Kiislamu ni kutakasa nyoyo na nafsi za wanadamu kupitia utaratibu maalumu ambao humuwezesha mwanadamu kuona na kujua mambo ambayo si rahisi kufahamika na watu wengine wa kawaida. Wamesema Qur'ani pia inazungumzia na kusisitiza juu ya suala hilo, ambalo linapasa kumpelekea mja kumuogopa zaidi Mwenyezi Mungu na kutii amri zake.
Mwishoni mwa kikao hicho kikao kingine cha mazungumzo ya fikra za kifalsafa na kiirfani kimefanyika ambapo wasomi wa Kiirani wamejibu maswali yaliyoulizwa na washiriki kuhusiana na elimu hizo mbili. 379552