IQNA

Baraza la Haki za Binadamu lapitisha azimio la kuzuia dharau dhidi ya dini

11:51 - March 28, 2009
Habari ID: 1758320
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa siku ya Alkhamisi lilipitisha azimio la nchi za Kiislamu la kuzuia kufanywa dharau dhidi ya matukufu ya kidini. Azimio hilo lililowasilishwa na Pakistan kwa niaba ya nchi za Kiislamu, lilipitishwa kwa kura 33 dhidi ya 11 zilizopinga.
Nchi za Magharibi ndizo zilizokuwa wapinzani wakubwa wa azimio hilo zikidai kwamba kupitishwa kwake ni ukiukaji wa misingi ya uhuru wa kusema.
Kwa msingi wa azimio hilo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapasa kufanya juhudi za kuzuia kutusiwa dini, ubaguzi dhidi ya wafuasi wa dini tofauti na uchochezi dhidi ya wafuasi wa dini hizo.
Azimio hilo limekosoa vikali dharau ya mara kwa mara inayofanywa dhidi ya Uislamu na kuhusishwa kwa dini hiyo tukufu na ugaidi pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu.
Kuhusiana na suala hilo, Dhamir Akram, Balozi wa Pakistan katika Baraza la Haki za Binadamu amesema, dharau dhidi ya dini na kuenezwa mitazamo potofu kuhusiana nazo hupelekea kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya wafuasi wa dini hizo na kwamba juhudi za lazima zinapasa kufanywa ili kuzua kabisa dharau hiyo.
Maazimio ya baraza hilo lenye makao makuu yake huko Geneva, hayana ulazima wa kutekelezwa kisheria na yanachukuliwa tu kuwa ushauri kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. 380564
captcha