IQNA

Askofu wa Canterbury asifu nafasi ya Uislamu katika jamii

12:06 - March 28, 2009
Habari ID: 1758324
Askofu Mkuu wa Canterbury, amesifu mchango wa Waislamu katika kuimarisha nafasi ya dini katika jamii ya Uingereza.
Kwa mujibu wa gazeti la Muslim News, Dakta Rowan Williams amesema katika mahojiano na gazeti hilo kwamba Uislamu na Waislamu wamekuwa na nafasi muhimu sana katika kuimarisha nafasi ya dini katika upeo mpana wa jamii.
Huku akikosoa kudhoofishwa kwa makusudi misingi ya maadili katika jamii za kimaada za leo, Dakta Williams amesisitiza udharura wa kuhuishwa misingi ya maadili, kuwajibika kwa watu katika utekelezaji wa majukumu yao katika jamii na kuimarishwa kwa uhusiano wao na Mwenyezi Mungu. Amesisitiza kwamba mwanadamu hawezi kuwa mkamilifu bila ya kuwa na uhusiano na Muumba wake, na kwamna jamii ya mwanadamu bila shaka itapata madhara makubwa kwa kudhoofishwa uhusiano huo.
Askofu Mkuu wa Canterbury pia ameridhishwa na kuimarishwa kwa mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo na kusema kuwa jambo hilo litapelekea kuelewana zaidi wafuasi wa dini mbili hizi za mbinguni. Akijibu swali kuhusiana na sababu ya kukaa kimya viongozi wa Kikristo na Kiyahudi kuhusiana na jinai zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko katika Ukanda wa Gaza, Dakta Rowan amesema katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo kwamba, ni jambo lisilokubalika kabisa kisheria kuuawa kwa raia wasio na hatia na kuongeza kwamba, hadhani kuwa kuna kiongozi yeyote wa kidini ulimwenguni anayeunga mkono jambo hilo.
Pia ameelezea kuwa tayari viongozi wa kidini wa Uingereza kwa ajili ya kutoa misaada ya kibinadamu kwa wahanga wa mauaji ya umati ya utawala wa kibaguzi wa Israel. 380570
captcha