Qur'ani moja inayohusishwa na Imam Musa Kadhim (as) imehifadhiwa huko katika mji wa Srinegar Kashmir. Gazeti la Rising Kashmir, limeashiria historia ya kuingia Qur'ani hiyo ambayo imeandikwa kwa hati za kikufi katika eneo hilo na kusema kuwa imehifadhiwa katika sehemu inayoitwa Babul Hawaij.
Ukarasa wa mwisho wa Qur'ani hiyo una muhuri unaonyesha tarehe 173 Hijiria. Inasemekana kuwa Imam kadhim (as) aliandika Qur'ani hiyo alipokuwa akihudumia kifungo cha jela kwa amri ya mtawala dhalimu Harun ar-Rashid.
Baada ya kuaga dunia Imam, Qur'ani hiyo ilihamishiwa Ardebil nchini Iran na kisha kupelekwa katika eneo la Kashmir mwaka 660 Hijiria na mtu aitwaye Sayyid Sultan Haidar Ghabrawi. Tokea wakati huo hadi sasa, Qur'ani hiyo ingali inahifadhiwa huko na kizazi cha mtu huyo. Qur'ani hiyo iliandaliwa sehemu maalumu ya kuihifadhi mwaka 1968. Mwaka uliofuata, kamati maalumu ya kuhifadhi Qur'ani hiyo ilibuniwa.
Licha ya kuwa karne 13 zimepita sasa tokea kuhifadhiwa huko Qur'ani hiyo bila ya kutumiwa mada zozote za kemikali, lakini hakuna mabadiliko yoyote yenye madhara ambayo yamekipata kitabu hicho kitakatifu wala kubadilika rangi iliyotumika kukiandika.
Watu hupewa siku mbili tu katika mwaka kutembelea na kukiona kwa karibu kitabu hicho kitakatibu, nazo ni siku za kumbukumbu ya kifo cha Imam Kadhim na pia tarehe 20 Swafar ambayo inasadifiana na Arbaini ya shahada ya Imam Hussein (as). 382211