Mashindano ya tano ya kimataifa ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu maalumu kwa wanajeshi yanayofanyika chini ya anwani ya Tuzo ya Kimataifa ya Amir Sultan bin Abdul Aziz, yalianza jana Jumamosi huko katika mji mtakatifu wa Makka.
Mashindano hayo yanayofanyika kwa usimamizi wa Amir Sultan bin Abdul Aziz, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri la nchi hiyo, yanawashirikisha watu 69 kutoka nchi 19 za Kiarabu na Kiislamu.
Mashindano hayo yataendelea kwa muda wa wiki moja na yamelenga kuwashajiisha wanajeshi wa nchi mbalimbali kuzingatia mafundisho ya Qur'ani.
Waandaaji wa mashindano hayo pia wamewapangia ratiba maalumu washiriki wa mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kutekeleza amali za umra, kuzuru maeneo matakatifu nchini Saudi Arabia ukiwemo mji mtakatifu wa Madina na pia kiwanda cha uchapishaji Qur'ani Tukufu cha Mfalme Fahd.
Maonyesho maalumu ya kuonyesha jinsi Saudi Arabia imekuwa ikichangia katika kueneza Uislamu ulimwenguni pia yataandaliwa pambizoni mwa mashindano hayo. 382968