IQNA

Waislamu wa Ufaransa wanapasa kushiriki katika shughuli za kijamii

13:33 - April 13, 2009
Habari ID: 1764154
Tariq Ramadhan, mhadhiri wa falsafa na utafiti wa Kiislamu amewataka Waislamu wa Ufaransa kulinda utambulisho wao na kushiriki vilivyo katika shughuli za kijamii nchini humo.
Akizungumza katika kongamano la sita la Waislamu wa Ufaransa ambalo hufanyika kila mwaka, Ramadhan ameashiria udharura wa Waislamu kujishughulisha na shughuli za kijamii nchini Ufaransa na kusisitiza kuwa licha ya udharura wa jambo hilo, Waislamu wanapasa kulinda utambulisho na itikadi zao za Kiislamu.
Amesema, Waislamu wa Ufaransa wanapasa kuwabainishia vyema wenzao wasio Waislamu mafundisho halisi ya dini hiyo ili kuwavutia wayafahamu zaidi mafundisho hayo na sio kuwatwisha na kuwalazimisha wayakubali. Huku akisoma aya za Qur'ani zinazosisitiza juu ya kuishi kwa amani wafuasi wa dini mbalimbali, msomi huyo amesisitiza kuwa licha ya kuhifadhi na kulinda itikadi zao za Kiislamu, Waislamu wanawajibika kuheshimu sheria za kijamii zilizobuniwa na serikali ya Ufaransa.
Akiashiria umuhimu wa Waislamu kutafuta elimu na kupata vyeti vya juu vya kielimu, mhadhiri Ramadhan amesema kuwa hakuna kizuizi chochote kinachowazuia Waislamu kufikia viwango vya juu zaidi kielimu na kwamba wana kila haki ya kuwa matajiri, kuwa na maisha bora na kunufaika na neema zote walizopewa na Mwenyezi Mungu kwa sharti kwamba wasilisahau tabaka la watu masikini na wahitaji katika jamii. 386672
captcha