IQNA

Marekani na Israel zinazusha hitilafu kati ya nchi za Kiislamu

22:47 - April 16, 2009
Habari ID: 1765742
Ayatullahil Udhmaa Makarim Shirazi amesema kuwa tuhuma zilizotolewa na serikali ya Misri dhidi ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon zinakidhi matakwa ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ayatullah Makarim Shirazi ambaye ni miongoni mwa wanazuoni wa ngazi za juu wa Qum nchini Iran amesema, Marekani na utawala ghasibu wa Israel ni maadui nambari moja wa Waislamu na zinaendelea kuikalia kwa mabavu Baitul Muqaddas na kibla cha kwanza cha Waislamu wote.
Amesema kuwa maadui daima wamekuwa wakifanya njama za kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya nchi za Kiislamu na kuzuia umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa dini hiyo. Ayatullah Shirazi amesema, nchi kama Saudi Arabia na Misri hazipaswa kuvuruga umoja na mshikamano wa Kiislamu hususan katika kipindi hiki ambapo mshikamano wa nchi za Kiislamu ni jambo la dharura.
Amesema tuhuma zilizotolewa na Misri dhidi ya harakati ya Hizbullah ni njama chafu za maadui ambao wanataka kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuzusha hitilafu kati ya nchi za Kiislamu. Amesisitiza kuwa wapiganaji shupavu wa Hizhullah walilinda heshima ya Waislamu kwa ushindi wao dhidi ya Wazayuni wa Israel katika vita vya siku 33 dhidi ya Lebanon na kuna ulazima wa harakati hiyo kulindwa na kutetewa. Amesema kuwa moja ya siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwalinda na kuwatetea Waislamu na kwamba Iran ilitoa mchango mkubwa zaidi wa kimaanawi kwa wananchi wa Gaza wakati wa mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya eneo hilo.
Ayatullah Shirazi ameashiria mashambulizi yanayofanywa na Mawahabi wenye misimamo mikali na Saudi Arabia dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na akasema Mawahabi hao wanawafanyia uhasama Waislamu kutokana na uchochezi wa Marekani na utawala ghasibu wa Israel.
Siku chache zilizopita serikali ya Misri iliituhumu Hizbullah kuwa imetuma wanachama wake nchini huko kutekeleza operesheni za uharibifu. 389042
captcha