Gazeti la Denmark la Jyllands-Posten ambalo mwaka 2005 lilichapisha vikaragosi vya kutusi na kumkosea heshima Mtume Muhammad (saw) pamoja na matukufu mengine ya Kiislamu na hivyo kuamsha hasira kubwa ya Waislamu ulimwenguni, limedai kwamba hasira hiyo ni dalili ya Waislamu kutostahamili itikadi za wapinzani wao.
Hayo yamedaiwa na mmoja wa wakuu wa gazeti hilo la kichochezi alipohojiwa na gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot alipokuwa akizungumza katika Chuo Kikuu cha Kiibrania huko katika mji wa Jerusalem. Amedai kwamba radiamali ya Waislamu kuhusiana na vikaragosi hivyo vya matusi dhidi ya matukufu ya Kiislamu inathibitisha kwamba wanataka kueneza na kutekeleza sheria za Kiislamu barani Ulaya.
Akijibu swali kuhusiana na sababu ya kuchapishwa vikaragosi hivyo mkuu huyo ametetea hatua hiyo ya dharau kwa kudai kwamba, gazeti hilo halikuwa na lengo la kuwaudhi Waislamu bali wakuu wake walitaka tu kutoa radiamali kuhusiana na sensa na uchujaji unaofanywa kuhusiana na masuala ya Kiislamu na eti kutotoa ruhusa ya kuwekwa vizuizi katika uhuru wa kusema na kujieleza.
Amesisitiza kuwa hajuti kuhusiana na nafasi yake katika kuchapisha vikaragosi hivyo na kuongeza kuwa jambo hilo linaweza kuhalalishwa katika msingi wa uhuru wa kusema. 392850