Mwakilishi wa Niger katika kikao cha kimataifa cha Waendesha Mashataka wa nchi za Kiislamu na wanasheria kilichomalizika hivi karibuni hapa mjini Tehran amesema kuwa uzembe wa Umoja wa Mataigfa na udhaifu wa siasa zake kuhusiana na utawala haramu wa Israel, ndiyo sababu kuu ambayo imeupelekea utawala huo kumea pembe na kuendelea kutekeleza mauaji na jinai dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Hayo yamesemwa na Othman Beido mmoja wa ujumbe wa waendesha mashtaka wa Niger. Amesema, miaka sitini imepita sasa tokea utawala haramu wa Israel uteke na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kwamba kwa masikitiko makubwa hakuna hatua zozote za maana ambazo zimechukuliwa na mashirika ya kimataifa na hasa Umoja wa Mataiafa katika kukabiliana na suala hilo na kuulazimisha utawala huo kuondoka katika ardhi za Wapalestina wala kutatua mzozo uliopo kati ya pande hizo. Kwa msingi huo, amesema kuwa Waislamu wanapasa kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika kuchukua hatua za kivitendo kwa lengo la kukabiliana na mauaji pamoja na jinai zinazotekelezwa na utawala huo wa Tel Aviv dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.
Othman Beido amesema uzembe wa Umoja wa Mataifa umeupelekea kutoa maazimio dhaifu na yasiyotekelezwa. Amesisistiza kwamba kama kweli umoja huo ulikuwa na lengo la kutatua mzozo wa Palestina na kuwasaidia wananchi wa Palestina bila shaka haungeruhusu kuuawa kwa umati wakazi wa Ukanda Gaza hivi karibuni katika hujuma ya kinyama iliyotekelezwa dhidi yao na utawala wa Israel. Amesema uzembe huo wa Umoja wa Mataifa umewapelekea watawala katili wa Israel kuendeleza jinai zao dhidi ya Wapalestina bila kujali lolote na kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya the Hague pia imeamua kukaa kimya kuhusiana na mashtaka yaliyowasilishwa kwake na pande mbalimbali husika. Amesema kwamba, nchi wanachama wa Umoja wa Nchi za Kiislamu OIC zinaweza kushirikiana na kutoa mashinikizo ya kimataifa kwa lengo la kufikishwa mahakamani watawala hao wa utawala wa Israel waliohusika na mauaji ya umati dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Othman Beido amesema, hata kama watawala hao hawajatia saini Azimio la Rome, lakini wanaweza kufikishwa makahamani kama walivyofanywa watawala wa Yugoslavia ya zamani ili kujibu mashtaka ya jinai dhidi ya binadamu. Amesisitiza kwamba matarajio hayo muhimu ya nchi za Kiislamu yanaweza kutimia tu kwa ushirikiano wao pamoja na wanasheria wa kimataifa. 393640