IQNA

Jumuiya ya Nchi za Kiislamu yalaani mashambulio ya kigaidi ya Kadhimain

10:29 - April 27, 2009
Habari ID: 1770124
Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC imetoa taarifa ikilaani vikali mashambulio ya hivi karibuni yaliyotekelezwa na magaidi karibu na haram ya Imam Musa al Kadhim (as) nchini Iraq, tukio la kigaidi ambalo lilipelekea makumi ya Waislamu wasio na hatia kupoteza maisha yao na wengine wengi kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Kuwait KUNA, Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ameeleza masikitiko yake makubwa na mshikamano wake na serikali pamoja na familia za wahanga wa tukio hilo la kigaidi katika kuomboleza wahanga wa mauaji hayo ya kinyama dhidi ya watu wasio na hatia, na kuwatakia faraja na nafuu watu waliojeruhiwa katika shambulio hilo.
Katibu Mkuu wa OIC vilevile ametuma salamu za rambirambi kwa serikali na taifa la Iran kutokana na kuwapoteza raia wake wengi katika tukio hilo la kigaidi, waliokuwa wamekwenda huko kwa ajili ya kuzuru maeneo matakatifu ya Iraq. Ameitaka serikali ya Baghdad kufanya jitihada zaidi kwa ajili ya kuimarisha usalama na uthabiti wa nchi hiyo.
Awali Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la OIC, ISESCO, lilitoa taarifa likilaani mashambulio hayo na kuwataka Waislamu wote kushirikiana na Iraq katika kumaliza kabisa vitendo vya ugaidi na utumiaji mabavu nchini humo. Wametakiwa kulaani wazi vitendo vya ugaidi na mabavu dhidi ya watu wasio na hatia ili kulinda usalama wa Iraq. 394552
captcha