IQNA

Kutotekelezwa sheria za kimataifa kunadhoofisha umuhimu wake

10:05 - April 27, 2009
Habari ID: 1770126
Kutotekelezwa sheria za kimataifa au baadhi ya wakati kutekelezwa kimaslahi sheria hizo dhidi ya baadhi ya nchi, ni jambo linaloonyesha kutokuwepo dhamana ya kutekelezwa kwa usawa sheria hizo katika upeo wa kimataifa.
Hayo yamesemwa na Amsto Susidibi, mhadhiri wa masuala ya sheria ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu na Amani la Chuo Kikuu cha Dakar ambaye alikuwa katika ujumbe wa Senegal katika kikao kilichomalizika hivi karibuni mjini Tehran cha Waendesha Mashtaka wa nchi za Kiislamu na wanasehria wa kimataifa.
Msomi huyo amesema kuwa kwa masikitiko makubwa tunashuhudia kwamba sheria za kimataifa zanapuuzwa na kutotekelezwa katika pemba mbalimbali za dunia na nyingine kutekelezwa kimaslahi dhidi ya baadhi ya nchi. Amesema kuwa kutoadhibiwa na kutochukuliwa hatua za kisheria watu wanaovunja sheria za kimataifa ni jambo linalopelekea sheria hizo kukosa umuhimu wake kiutendaji.
Amsto Susidibi amesisitiza kwamba sheria zote za kimataifa zinapaswa kutekelezwa kwa usawa kwa watu wote bila ya kundi, chama wala nchi yoyote kutumia vibaya sheria hizo kwa maslahi yake binafsi.
Huku akiashiria matukio machungu ya mashambulio ya kinyama yaliyotekelezwa hivi karibuni na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia huko katika Ukanda wa Gaza, Amsto Susidibi amesema, picha za kutisha za watoto na wanawake waliouawa kinyama katika tukio hilo zilithibitisha udharura wa kutekelezwa kwa uadilifu sheria za kimataifa dhidi ya wahalifu wanaotekeleza jinai za kivita dhidi ya binadamu.
Msomi huyo wa Senegal amesema kuwa kimya cha jamii ya kimataifa, kuhusiana na hujuma hiyo ya kinyama ya siku 22 ya Israel kilikuwa alama ya njama, na kusisitiza masikitiko yake makubwa kwamba jambo hilo linathibitisha wazi kuwa jamii hiyo haina mtazamo mmoja kuhusiana na jinai za wazi zilizotekelezwa dhidi ya wakazi wa Gaza, na kwamba jambo hilo linatoa mwanya wa madola makubwa duniani kuingilia sheria za kimataifa kwa madhara ya utekelezwaji sheria za kiadilifu ulimwenguni.
Amesema, kwa kutilia maanani ukweli huo mchungu, mashirika na nchi za Kiislamu zinaweza kushirikiana na kuwa nguvu kubwa duniani kwa maslahi ya utekelezwaji kiuadilifu sheria za kimataifa. 394131
captcha