Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Qur'ani ya Oxford nchini Uingereza Muhammad Jawad Jauhar ambaye ameshiria mkutano wa Qur'ani Tukufu uliopangwa kufanyika tarehe 17 Agosti mwaka huu katika Chuo Kikuu cha Oxford na akasema kuwa mkutano huo ni katika juhudi za kuarifisha nafasi ya Qur'ani katika zama za sasa na kueleza njia za kustawisha nafasi ya sasa ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na kujibu changamoto mbalimbali zinazokikabili.
Jawad Jauhar amesema: Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kudhihiri kwa serikali ya kiislamu, Uislamu ulipata nafasi maalumu katika medani ya siasa ambapo wale waliokuwa wakipinga serikali ya kidini walizidisha changamoto zao dhidi ya Uislamu, Waislamu na Qur'ani. Amesema wimbi hilo la changamoto za kuupinga Uislamu na Qur'ani limeshadidi zaidi baada ya matukio ya miaka ya hivi karibuni nchini Marekani.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Oxford amesema kuhusu wajibu wa Waislamu katika zama za sasa kwamba katika zama hizi ni wajibu wa Waislamu kurekebisha tabia na mwenendo wao kwa kuiga mafundisho ya Qur'ani ili maneno yao yaweze kuwa na taathira. Ameongeza kuwa katika zama za mapinduzi ya vyombo vya mawasili kuna haja ya kuarifisha Qur'ani na mafundisho yake kupitia vyombo mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kipindi hiki, kwani iwapo watu wataelewa vyema sura halisi ya Qur'ani na mafundisho yake hawatakubali tena urongo na uzushi mwingi unaotolewa kuhusu kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. 394912