Kwa mujibu wa tovuti ya Islamonline, ikitoa taarifa kuhusiana na suala hilo, Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa utawala wa Israel unapasa kusimamisha mara moja operesheni ya kubomoa nyumba za Wapalestina na kuandaa mpango wa kumaliza mgogoro wa nyumba za Wapalestina wanaoishi Baitul Muqaddas.
Kila mwaka maafisa wa Utawala wa Israel hubomoa nyumba nyingi za Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo kwa kisingizio cha kutokuwa na vibali vya ujenzi. Tokea eneo la Baitul Muqaddas likaliwe kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel mwaka 1967, ubomoaji nyumba umekuwa sehemu muhimu ya siasa za utawala huo kwa lengo la kuwafukuza Wapalestina katika mji huo mtakatifu na kuufanya kuwa wa Kiyahudi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa, uharibifu huo wa nyumba za Wapalestina haumalizikii katika eneo la Beitul Muqaddas tu, bali mabuldoza ya utawala huo yanajiandaa kuharibu nyumba nyingine za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, iwapo utawala wa Israel utatekeleza uamuzi wa kuendelea kubomoa nyumba za Wapalestina, uamuzi ambao tayari umethibitishwa na mahakama za utawala huo, Wapalestina wapatao 60,000 watapoteza makazi yao. 398075