IQNA

Siasa za Israel huko Quds ni mauaji ya kizazi

17:59 - May 09, 2009
Habari ID: 1775773
Kundi moja la wanasiasa wa Misri lilitoa taarifa siku ya Ijumaa likisema kuwa hatua zinazotekelezwa na askari wa utawala haramu wa Israel huko Quds kwa lengo la kufuta athari za Kiarabu na Kiislamu katika mji huo mtakatifu na pia kuufanya uonekane kuwa ni wa Kiayahudi zinatekelezwa kwa lengo la kukifuta kabisa kizazi cha Wapalestina katika mji huo.
Kwa mujibu tovuti ya al-Arabonline, taarifa hiyo inazitaka nchi zote za Kiarabu na wapigania uhuru kote ulimwenguni kuchukua hatua za dharura kwa lengo la kusimamisha mara moja hatua hizo hatari za utawala wa Kizayuni. Taarifa hiyo inasema kuwa ukweli wa mambo na takwimu za kutisha zinaelezea kuongezeka vitendo vya jinai za Wazayuni dhidi ya wakazi wa Quds na raia wa Kipalestina katika siku za hivi karibuni na kwamba mpango wa kiuadui na chuki wa utawala haramu wa Israel wa kuufanya mji wa Quds kuwa wa Kiyahudi umefikia kilele. Taarifa hiyo inaashiria mpango wa Wazayuni wa kuwafukuza wakazi wa Kipalestina kutika katika mji wa Quds kwa kubomoa ovyo nyumba zao, na kuongeza kuwa mpango wa utawala huo wa kujenga hekalu la Mayahudi mahala pa Msikiti wa al-Aqsa ni msiba mkubwa kwa Waarabu na Waislamu. Imesema kuwa kuendelea kwa vitendo vya uharibifu wa msikiti huo kwa lengo la kujengwa hekalu lililotajwa ni hatari kubwa kwa utambulisho wa Kiislamu na Kiarabu wa eneo hilo. Katika taarifa hiyo, wanasiasa wa Misri wamesisitiza kwamba mapambano ya wananchi dhidi ya ukandamizaji na jinai za Wazayuni wa Israel ni wadhifa wao wa kisheria, kimaadili, kiutu na kitaifa. Wamezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kuushinikiza utawala wa Kizayuni kusimamisha haraka vitendo vyake vya kibaguzi dhidi ya Wapalestina na kukata kabisa uhusiano wao wa kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi na utawala huo haramu. Katika taarifa hiyo wanasiasa wa Kiarabu walitangaza siku ya Ijumaa ijayo tarehe 15 Mei kuwa siku ya hasira ya ulimwengu na mataifa ya Kiislamu na wapigania uhuru duniani dhidi ya unyama wa Wazayuni na kuwataka Waislamu kulinda umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na Wazayuni na waungaji mkono wao na vilevile nchi zote zinazoshirikiana na utawala huo haramu. Wakati huohuo, Taasisi ya Haki za Kijamii na Kiuchumi ya Quds imetangaza kuwa tokea kuingia madarakani Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Israel, utawala huo umezidisha kasi ya kuharibu makazi ya Wapalestina huko Quds kwa lengo la kuufanya mji huo mtakatifu kuwa wa Kiyahudi.
401622

captcha