IQNA

Imam Khomeini (MA) aliwapa nguvu Waislamu duniani

7:05 - June 07, 2009
Habari ID: 1787858
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Alkhamisi Juni 4, 2009 amehutubia umati mkubwa wa watu wa matabaka mbalimbali wa ndani na wa nje ya nchi walioshiriki katika maadhimisho ya 20 ya kukumbuka siku aliyofariki dunia mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye).
Ayatullah Khamenei amesema katika maadhimisho hayo kwamba kupeperushwa hewani bendera mbili za "kuuhuisha Uislamu" na "kuiletea heshima Iran na Uirani" ni vipengee viwili vikuu vya harakati ya kihistoria ya Imam Khomeini (MA). Aidha ameashiria njama zinazofanywa na maadui za kukwamisha maendeleo ya taifa la Iran na kusisitiza kuwa, wananchi wote na kila anayependa kuuona mfumo wa utawala wa Kiislamu unaimarika nchini anapaswa kushiriki kwa nguvu zake zote katika uchaguzi wa Rais wa tarehe 12 Juni mwaka huu.

Vile vile ametoa mkono wa pole kwa kumpoteza baba wa taifa la Iran yaani Imam Khomeini (MA) na kuongeza kuwa, miongoni mwa matunda bora kabisa ya kupeperushwa bendera ya kuuhuisha Uislamu kulikofanywa na Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) ni kuwafanya Waislamu duniani wapate nguvu za kujivunia utambulisho wao na kuitetea vilivyo dini yao. Amesema mfano wa matunda mazuri ya mwamko huo ulioletwa na Imam Khomeini ni kulifanya taifa la Palestina lizinduke na kupata nguvu mpya baada ya kupita miaka mingi ya kuzorota, aidha harakati hiyo ya Imam Khomeini imeyafanya mataifa ya Kiarabu yapate matumaini mapya baada ya kushindwa mara kwa mara na vile vile kuufanya utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni donda la kensa katika kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu, uchezee kipigo mtawalia kutoka kwa vijana wa Kiislamu licha ya kwamba kabla ya hapo utawala huo ghasibu ulikuwa umejijengea sifa batili ya kuwa na nguvu zisizoshindika.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia Intifadha za mfululizo za wananchi wa Palestina na vipigo vya mara kwa mara unavyopata utawala wa Kizayuni wa Isrel, kukimbia kwa madhila utawala huo ghasibu katika maeneo ya kusini mwa Lebanon na kushindwa kwake katika vita viwili vya siku 33 vya nchini Lebanon na vya siku 22 vya Ghaza na kuongeza kuwa, mafanikio yote hayo yamepatikana kwa baraka za harakati ya Imam Khomeini aliyepeperusha bendera ya Uislamu kadiri kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel umelazimika kuachana kwa muda na kaulimbiu yake ya kuyateka na kuyatawala maeneo yote yaliyoko baina ya mito mwili ya Nail na Furati.

Ayatullah Khamenei amesema, juhudi za mataifa ya Kiislamu za kutaka yatawaliwe na serikali za Kiislamu, kupatikana moyo wa matumaini miongoni mwa wasomi na wanafikra wa ulimwengu wa Kiislamu na kulegezwa misimamo ya ulimwengu wa Magharibi mbele ya Waislamu, yote hayo yamepatikana kwa baraka za mwamko wa umma mzima na istikama inayoshuhudiwa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Amesisitiza kuwa, Waislamu kote ulimwenguni wanapaswa kujua thamani ya uzoefu huo wenye faida na manufaa mengi na kuendeleza njia yake ya haki kwa msingi wa uzoefu huo kwani amesema njia pekee ya kuweza mataifa ya Kiislamu kupata heshima na hadhi yake ni istikama.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusu kulegezwa misimamo ya nchi za Magharibi kuhusiana na mataifa ya Kiislamu na juhudi za nchi hizo za kujaribu kuwa na sura mpya mbele ya Waislamu kuwa, ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba, mabadiliko katika nchi hizo za Magharibi hayawezi kuja kwa maneno matupu bali inabidi maneno hayo yatekelezwe kivitendo na vifutwe vitendo vyote vya huko nyuma vya Marekani vya kupora haki za taifa la Iran na za mataifa mengine ya eneo la Mashariki ya Kati.

Ayatullah Udhma Khamenei amekumbusha kuwa serikali iliyopita ya Marekani ilidhihirisha sura ya chafu, ya ukatili na ya kuchukiza mno ya Marekani kutokana na vitendo vyake vya ukandamizaji, uingiliaji wa kijeshi katika mataifa mengine ya dunia, ubaguzi na kujiingiza mara kwa mara katika mambo yasiyoihusu. Amesema ni kwa sababu hiyo ndio maana Waislamu wanaichukia vibaya sana Marekani.

Amesema Marekani inadai kuguswa na hali ya kidemokrasia katika mataifa mbalimbali duniani lakini lilipofika suala la Wapalestina ambao walitumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wanaowapenda, Marekani ilisahau madai yake yote ya kutetea demokrasia na badala yake ikaendelea kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni katika kuwadhulumu Wapalestina na kuvuruga uamuzi wa kidemokrasia wa wananchi wa taifa hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia misimamo ya Marekani kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran na kuongeza kuwa, Marekani inaenezo uongo na kuficha ukweli kuhusiana na haki ya taifa la Iran ya kustafidi na teknolojia ya nyuklia katika masuala mbalimbali ya amani, na inadai kwamba Iran inataka kutengeneza bomu la atomiki.

Ayatullah Khamenei amesema kwa mara chungu nzima viongozi na taifa la Iran limekuwa likisema kwa uwazi kwamba suala la kutengeneza silaha za nyuklia halimo kabisa katika ratiba za kujilinda za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hata imesemwa wazi kwamba silaha za atomiki ni haramu kwa mtazamo wa sheria za Kiislamu lakini Wamagharibi na hasa hasa Marekani wanaendelea kueneza uongo wakidai kuwa Iran inataka kutengeneza bomu la nyuklia. Kwa kweli kufanya hivyo ni kuvunja wazi wazi haki za taifa la Iran, amesema.

Vile vile ameashiria siasa za Rais aliyepita wa Marekani aliyezivamia nchi za Afghanistan na Iraq kwa madai ya kupambana na ugaidi na kusisitiza kuwa, mtu anaweza kuamini matamshi ya viongozi wa Marekani pale tu viongozi hao wanapotekeleza kivitendo wanachokisema vinginevyo hakuna yeyote anayeweza kuamini maneno yao hata wakisema mamia kwa mamia ya maneno matamu kwa ajili ya Waislamu na hata wakitoa mamia kwa mamia ya hotuba za kuvutia kwa ajili ya ulimwengu wa Kiislamu.

Aidha amesema kipengee kingine cha harakati adhimu ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) ni kufufua moyo wa heshima na utukufu wa Iran na Uirani na kuongeza kuwa, Imam alibatilisha tabia ya kujihisi duni iliyopandikizwa na tawala vibaraka, za kibeberu na wasomi wa Magharibi nchini na badala yake akalipa uhai mpya taifa la Iran na akawafanya wananchi wa taifa hili kuwa na moyo wa kujiamini na kulithibitishia taifa la Iran kwamba linaweza kujitegemea na halishindwi na chochote.

Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia suala la maendeleo akisema kuwa nguvu kuu ya maendeleo na uwezo hasa wa taifa unatokana na mambo ya kimaanawi ya taifa hilo hususan kuwa na moyo wa kujiamini na kulinda heshima ya taifa mambo ambayo huziwezesha tawala zinazochaguliwa kidemokrasia na wananchi kuwa imara na madhubuti mbele ya mabeberu na hulifanya taifa lolote lenye sifa hizo, kuwa na nguvu katika milingano ya siasa za kimataifa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kuwategemea wananchi katika maongozi ya nchi, kujitosheleza, kuwa na nguvu katika miamala ya kiuchumi, kuzalisha elimu, kuwa na nafasi kubwa katika uzalishaji elimu duniani na kujivunia utamaduni, mila na desturi za taifa ni miongoni mwa mambo ambayo yanaipa maana halisi heshima ya taifa.

Amesema hatua ya kila mmoja kumuheshimu mwenzake ndiyo maana ya kivitendo ya heshima ya taifa katika uongozi wa jamii na kuongeza kuwa, heshima ya taifa katika siasa za nje ina maana ya kuwa na uhuru wa kusema kwa namna ambayo kusiwe na dola lolote litakaloweza kulitwisha na kuliburuza taifa husika katika jambo lolote lile.

Amekumbusha kuwa harakati ya miaka 30 ya taifa la Iran imekumbana na hali mbalimbali lakini haijawahi kusimama hata mara moja. Amesema taifa lenye ufahamu mpana la Iran linalinda heshima yake katika nyanja zote na linaendeleza njia yake ya kufikia daraja za juu ya maendeleo kwa uwezo na nguvu kamili. Ameongeza kuwa kuna siku taifa la Iran litafikia hatua ambayo maadui hawatathubutu tena kuleta choko choko na vitisho vyovyote dhidi yake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa athari njema za heshima ya taifa kubwa la Iran zinashuhudiwa wazi katika masuala mbalimbali duniani na kwamba maneno ya watu ambao wanadai Iran imepoteza nafasi na heshima yake duniani kutokana na kutotetereka katika misimamo yake, hayana ukweli hata chembe.

Ameongeza kuwa, maadui wanaofanya ubeberu na kuingilia mambo ya Jamhuri ya Kiislamu na ambao wameunda kambi maalumu dhidi ya taifa la Iran wanaendesha propaganda kubwa ili kulifanya taifa hili lijione duni lakini ukweli wa mambo ni kuwa, heshima ya taifa kubwa la Iran na Imam Khomeini MA imejikita hata ndani ya nyoyo za maadui wa mfumo wa utawala wa Kiislamu wa Iran.

Ayatullah Udhma Khamenei amesema kwamba kujiweka mbali na wananchi, kutojali matukufu ya Kiislamu na kusahau njia tukufu ya Imam Khomeini ni hatari kubwa kwa taifa la Iran. Amesema: "Inabidi tusonge mbele wa nguvu zote hadi ushindi wa mwisho kupitia kulinda misingi madhubuti ya mfumo wa utawala wetu ambao ni kumbukumbu ya Imam wetu azizi na kwa kutegemea hima ya wananchi hususan vijana."

Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia nukta nne muhimu kuhusiana na uchaguzi muhimu mno wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaotarajiwa kufanyika tarehe 12 mwezi huu wa Juni.

Ameashiria katika nukta ya kwanza kwamba baadhi ya wakati maadui wa taifa la Iran wanaziita chaguzi za Iran kuwa ni za kuteuliwa tu wakijaribu kuonyesha kuwa wananchi hawana nafasi yoyote katika kuchagua viongozi wao. Baadhi ya wakati wanadai ushindani uliopo baina ya wagombea ni mchezo tu wa kisiasa unaoongozwa kutoka ndani ya serikali na kwamba eti lazima kutafanyika udanganyifu tu katika uchaguzi. Amesema lengo la propaganda zote hizo ni kuuharibu mfumo wa demokrasia ya kidini unaotawala nchini Iran na kuwakatisha tamaa wananchi wasijitokeze kwa wingi katika chaguzi.

Ayatullah Khamenei pia amesema taifa la Iran ni taifa la watu wenye akili nyingi, walio macho na waliopevuka na kuongeza kuwa, adui anafanya njama za kutaka kuupokonya mfumo wa utawala wa Kiislamu nchini nguvu yake muhimu nayo ni uungaji mkono wa wananchi. Amesema anasikitishwa mno kuona kwamba kuna baadhi ya watu ndani ya nchi wamekumbwa na mghafala na wanakariri na kurejea maneno yale yale yanayotolewa na maadui na hivyo kusaidia kivitendo njama za kufanikishwa malengo ya maadui hao.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, miongoni mwa mambo ambayo wananchi wa Iran wanajivunia ni kuwa na haki ya kuchagua viongozi wa sekta mbalimbali nchini na kuongeza kuwa, maadui wa kigeni wanafanya njama za kuwapora wananchi wa Iran fursa na fakhari yao hiyo lakini mtu yeyote anayependa kuona mfumo huu wa utawala na dini ya Kiislamu na taifa la Iran linaimarika na kupata nguvu ni wajibu kwake kiakili na kisheria kushiriki katika kupiga kura.

Katika nukta ya pili ya mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba kujitokeza wagombea mbalimbali wenye mitazamo na mbinu tofauti wanaoungwa mkono na makundi mbalimbali ya wananchi katika chaguzi zinazofanyika nchini Iran ni miongoni mwa fakhari na mambo ya kujivunia ya mfumo wa utawala wa Kiislamu nchini. Hata hivyo amewataka wafuasi wa vyama na wagombea tofauti wasitumie vibaya hitilafu zao za mitazamo kwani jambo hilo linaweza kutumiwa vibaya na maadui dhidi yao wote.

Nukta ya tatu aliyoigusia kuhusiana na uchaguzi ujao wa Juni 12, imewahusu wagombea wenyewe katika uchaguzi huo akisema si sahihi na haijuzu mgombea kutumia maneno mabaya na kuonyesha uadui dhidi ya mgombea mwenzake kwa ajili ya kujiuza kwa wananchi.
Amesema yeye binafsi yake hapingi suala la kuweko mdahalo baina ya wagombea, lakini kila mmoja anapaswa kuchunguza sheria na mafundisho ya dini katika kampeni zake na ajue kwamba wananchi wako macho na wanajua vyema lililo zuri na baya.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa kutofautiana kifikra na kimitazamo katika mambo mbalimbali ni jambo la kawaida lakini inabidi wakati wagombea na wafuasi wao wanapozungumzia masuala ya uchaguzi na wanapotoa hoja zao dhidi ya wagombea wengine watoe hoja hizo kwa namna ya udugu na kupendana bila ya kuleta vurugu zozote.

Amma katika nukta ya nne na ya mwisho ya hotuba yake hiyo kuhusu uchaguzi, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amekumbusha kwa mara nyingine tena kwamba yeye hana isipokuwa kura yake moja na mtu hawezi kujua atampigia nani kura na amesema hamwambii mtu yeyote mgombea aliyemchagua. Vile vile amesema hamwamrishi mtu yeyote aende kumchagua mgombea gani na asimchague mgombea gani kwani jambo hilo amesema linawahusu wananchi wenyenwe na linalihusu taifa.

Akifunga hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, anachowaomba wananchi ni kwamba wajitokeze kwa wingi na kwa nguvu zao zote katika uchaguzi ujao wa tarehe 12 mwezi huu wa Juni kwa ajili ya kumchagua Rais wa baadaye wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
http://www.khamenei.ir/
416123
captcha