IQNA

Kuanzishwa jumba la makumbusho ya mambo ya kale ya Qur'ani nchini Uturuki

12:52 - August 24, 2010
Habari ID: 1979996
Jumuiya ya Marafiki wa Qur'ani Tukufu ya Uturuki imeazimia kuanzisha jumba maalumu la makumbusho ya athari na mambo ya kale kuhusu Qur'an ikiwa ni katika ratiba ya shughuli zake za mwaka huu wa 2010.
Kwa mujibu wa gazeti la Uturuki la Zaman, habari hiyo imetangazwa na Ahmad Sisman, msemaji wa jumuiya hiyo ambaye ameongeza kwamba kufuatia kutangazwa mwaka wa 2010 kuwa ni mwaka wa Qur'ani Tukufu, jumuiya hiyo ina mipango kadhaa muhimu ambayo itawatangazia mabalozi na wawakilishi wa kidini na kisiasa wa nchi za kigeni wanaoziwakilisha nchi zao nchini Uturuki katika karamu ya futari iliyopangwa kufanyika tarehe 5 Septemba. Ameendelea kusema kuwa moja ya mipango hiyo muhimu ni kuzinduliwa kwa jumba la maonyesho ya athari na mambo ya kale kuhusiana na Qur'ani Tukufu.
Mambo na vitu vitakavyoonyeshwa katika jumba hilo ni pamoja na athari na vitabu vyote vinavyohusiana na Qur'ani vikiwemo vitabu vya mafunzo na historia ya Qur'ani Tukufu, nakshi, utumiaji dhahabu katika nakshi na nuskha za Qur'ani zilizoandikwa kwa mkono.
Ameongeza kuwa mambo mengine yatakayoonyeshwa katika jumba hilo ni tarjumi mbalimbali za Qur'ani pamoja na chapa za kitabu hicho kitakatifu zilizochapishwa katika nchi mbalimbali za Kiislamu na zisizo za Kiislamu.
Ahmad Sisman amemaliza kwa kusema, kuandaliwa maonyesho ya kitaifa na kimataifa ya Qur'ani Tukufu ni baadhi ya mipango maalumu ambayo itatekelezwa katika jumba hilo la maonyesho ya mambo ya kale. 640238
captcha