Akizungumzia suala hilo katika maonyesho hayo hapo jana Jumapili, Hujjatul Islam wal Muslimeen Rabbani, Mshauri wa Masuala ya Kimataifa wa Taasisi ya Kimataifa ya Jamiatul Mustafa (saw) amesema kuwa uzingatiaji Qur'ani umeimarika zaidi katika nchi za Latin Amerika kutokana na juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema licha ya kuwa wahajiri kutoka nchi za Lebanon na Syria kabla ya hapo pia walitoa mchango katika kueneza Uislamu katika nchi hizo ambazo rai wao wengi ni Wakristo, lakini hujuma ya utamaduni wa nchi za Magharibi na kutokuwepo wanazuoni pamoja na vituo vya kidini katika nchi za Latin Amerika ni mambo yaliyowafanya Waislamu wa nchi hizo kuendelea kuishi katika hali ya udhaifu na kuwa jamii ya wachache.
Amesema kutokana na maneno ya Imam Khomeini (MA) kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulikuwa mlipuko wa nuru, nuru ya mapinduzi hayo iliwafikia watu wa nchi hizo za Latin Amerika na kwamba hivi sasa kuna vituo vya Kiislamu katika zaidi ya nchi 20 za eneo hilo, vituo ambavyo vina uhusiano wa karibu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kutumwa wasomaji Qur'ani na walinganiaji dini katika nchi za Latin Amerika, kutangazwa mafundisho ya kidini, usomaji na tafsiri ya Qur'ani kupitia redio na televisheni za nchi hizo ni baadhi tu ya shughuli zinazotekelezwa na Jamiatul Mustafa (saw) katika eneo hilo la Latin Amerika. 644484