Kwa mujibu wa gazeti la kimataifa la Darul Hayaat, matamshi hayo yametolewa na Abdul Aziz bin Othman al-Tuwaijri, Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO, katika kujibu ubezaji wa kundi la Wakristo na makasisi walio na misimamo ya kupindukia mipaka nchini Marekani ambao hivi karibuni walichukua hatua ya dharau dhidi ya Qur'ani Tukufu kwa kuichoma moto.
al-Tuwaijri amesema kupitia gazeti hilo kwamba, hatua za kiuadui na mashambulio dhidi ya Qur'ani hayajalenga Uislamu na Waislamu tu bali yamelenga amani, jamii zote na usalama wa dunia nzima. Amesema mashambulio hayo yanavuruga juhudi zote zilizofanyika katika miaka ya huko nyuma katika ngazi za kimataifa kwa madhumuni ya kuimarisha mazungumzo baina ya dini, tamaduni na staarabu mbalimbali.
Ametahadharisha kuwa ulimwengu utaendelea kushuhudia vitendo kama hivyo vya kuikosea heshima Qur'ani katika nchi za Magharibi iwapo siasa za chuki na makundi yenye misimamo ya kupindukia mipaka yataruhusiwa kuendesha shughuli zao za chuki dhidi ya dini na tamaduni nyingine bila kudhibitiwa.
al-Tuwaijri ameshangazwa na hali ya kuwa licha ya kuwa malalamiko mengi yamekuwa yakifanyika katika pembe mbalimbali za dunia kulaani dharau hiyo dhidi ya matukufu ya Kiislamu, lakini Papa Benedict wa XVI na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Kikristo wamenyamaza kimya bila kusema lolote kuhusiana na jambo hilo la aibu. 654592