Kwa mujibu wa tovuti ya Idaho Mountain Express, suala hilo limebainishwa wazi na Askofu Bob Henley wa Kanisa la Protestanti la Big Wood katika jimbo la Idaho ambaye ameongeza kuwa, kwa kitendo chake hicho cha dharau dhidi ya Qur'ani, Kasisi Jones amekiuka wazi misingi ya uhuru wa kusema na hivyo kuanzisha wimbi kubwa la fitina na ubaguzi wa rangi, wimbi ambalo limezusha mifarakano na hitilafu kubwa katika jamii ya wanadamu.
Huku akisisitiza kwamba Nabii Isah (as) amewataka wafuasi wake kuamiliana vyema na watu jinsi wanavyapenda wao waamiliana nao, Askofu Henley ameongeza kuwa kuchomwa Qur'ani mbele ya Waislamu ni kitendo cha kukera na kuchukiza sawa na ilivyo kuchomwa Injili mbele ya Wakristo. Amesema vitendo viwili hivyo ni vya dharau na kwamba watu wanapasa kuepuka dharau dhidi ya matukufu ya kidini.
Henley amesema, kitendo cha Jones na watu wengine wachache nchini Marekani cha kubeza Qur'ani kitapelekea kuongezeka vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu ulimwenguni. Amesisitiza kwamba kitendo hicho kimetekelezwa kwa shabaha ya kuzidisha uadui na ugomvi miongoni mwa watu jambo ambalo amesema linakwenda kinyume kabisa na mafundisho ya Isah au kwa jina jingine Yesu Kristo (as). 655793