Kwa mujibu wa tovuti ya Nun, maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wanafikra, wasomi, wasanii, waandishi, wanahistoria na wanazuoni mashuhuri wa Iraq. Madhimisho hayo yalifanyika chini ya anwani ya 'Baqee na Samarra, Bendera za Ashuraa.'
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Sayyid Adnan Jolokhan, mmoja wa mahatibu mashuhuri wa Iraq amesema kuwa vikao na mikutano inayofanyika kwa ajili ya kukumbuka tukio hilo chungu katika historia ya Kiislamu ni fursa ya kubainishwa huzuni na machungu ya Washia kuhusiana na uharibifu na msiba huo mkubwa. Amesema, mbinu na fikra hatari ya kukufurisha Waislamu wengine ambayo inatumiwa na kundi potofu la Mawahabi katika kuharibu makaburi ya Baqee na makaburi mengine ya Waislamu ni jambo hatari sana.
Ali Kadhim Sultan, mkuu wa Redio ya Haram ya Imam Hussein (as) pia alizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu hiyo na kusema kuwa fikra ya kukufurisha Waislamu wengine inayotumiwa na kundi hilo linalodai kuwa la Kiislamu ni hatari kubwa kwa misingi ya Uislamu na umoja wa umma mzima wa Kiislamu.
Amesema jinai ya kundi hilo ovu haiishii kwenye ubomoaji wa makuburu ya Maimamu watukufu (as) huko Baqee tu bali imeenea hadi kwenye umwagaji damu ya Waislamu wasio na hatia na kuhalalisha uporaji wa mali zao. Amesema maovu hayo ya Mawahabi yameharamishwa moja kwa moja na Qur'ani Tukufu pamoja na hadithi za Bwana Mtume (saw) na kwamba linahatarisha umoja wa umma wa Kiislamu.
Mawahabi walivamia na kuharibu makaburi ya Baqee ambapo Maimamu Watoharifu na masahaba wa Mtume Mtukufu (saw) wamezikwa, tarehe 8 mwaka 1344 Hijiria.
Waislamu wa madhehebu ya Shia huandaa vikao maalumu kila mwaka kwa ajili ya kukumbuka tukio hilo chungu na la kusikitisha katika historia ya Kiislamu. 658758