IQNA

Malalamiko ya kukosewa heshima Qur'ani nchini Marekani yaendelea Uturuki

17:07 - September 21, 2010
Habari ID: 1998849
Malalamiko makubwa yamekuwa yakiendelea katika miji tofauti ya Uturuki kufuatia hatua ya baadhi ya watu nchini Marekani kukosea heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu, Qur'ani.
Maandamano ya hivi karibuni kabisa yamefanyika katika mji wa Aydin ilioko katika mkoa wa kati wa nchi hiyo. Washiriki wa maandamano hayo ambayo yamewashirikisha malaki ya wakazi wa mji huo, wamepiga nara za kulaani vikali kitendo hicho cha dharau dhidi ya Qur'ani. Waandamanaji wametoa taarifa mwishoni mwa maandamano hayo wakisema kuwa kitendo hicho cha dharau kimewaudhi Waislamu wote katika ulimwengu wa Kiislamu. Licha ya kuwa Terry Jones wa kanisa la jimbo la Florida alifutilia mbali wito wake wa kutaka kuchomwa Qur'ani nchini Marekani kwa mnasaba wa kukumbukwa tukio la Septemba 11, lakini baadhi ya watu waliendelea mbele na uamuzi wao wa kuchoma moto kitabu hicho kitakatifu kwa kisingizio cha kuitikia wito wa kasisi huyo muovu.
Taarifa hiyo imesema kuwa Waislamu wanaoamini kuwa kitabu hicho ni muujiza wa milele wa Mtume Mtukufu (saw) hawawezi kukaa kimya mbele ya dharau hiyo na kwa hivyo wanawataka walimwengu wote badala ya kuchana na kukichoma moto kitabu hicho wachukue hatua ya kukisoma angaa mara moja kwanza, kisha wachukue uamuzi wao wa mwisho.
Imewataka wapinzani walio na uadui dhidi ya Uislamu ambao kila siku hupanga na kutekeleza njama za kuzuia kuenea mafundisho ya Kiislamu katika pembe mbalimbali za dunia, wafahamu vyema kwamba ustaarabu na utamaduni wanaonufaika nao hii leo unatokana na Uislamu na kwa hivyo waachane na uadui wao huo na kuikubali hakika iitwayo Qur'ani. 659618
captcha