Kwa mujibu wa shirika la Jahan la Uturuki, kufuatia tangazo la kasisi Terry Jones wa jimbo la Florida Marekani la kutangazwa siku ya tarehe 11 Septemba kuwa siku ya kimataifa ya kuchomwa moto Qur'ani Tukufu, kundi moja la raia wa Uingereza hivi karibuni lilichukua hatua ya kuchoma moto kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na kisha kusambaza picha zake kwenye tovuti mbalimbali za intaneti.
Picha hizo zimeamsha hasira ya Waislamu wa Uingereza, ambapo polisi ya nchi hiyo imetangaza kuwa umewatia nguvuni watu sita waliohusika na kitendo hicho ambacho imekitaja kuwa ni cha uhalifu kutokana na kuwa kinadharau itikadi na kueneza ubaguzi wa rangi.
Hata hivyo imesema, watu hao wameachiliwa huru kwa dhamana na kwamba wanasubiri tarehe ya kufikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili.
Vilevile viongozi wa kidini wa Uingereza wamelaani kitendo hicho na kusisitiza kwamba hakiakisi kwa njia yoyote ile msimamo rasmi wa wananchi wote wa Uingereza. 661526