Taarifa ya kikao hicho kilichofanyika katika Kituo cha Kiislamu cha Uingereza imeakisi mitazamo na nasaha za wanafikra na wasomi wa madhehebu tofauti za Kiislamu walioshiriki katika kikao hicho. Taarifa hiyo imewataka Waislamu wote duniani kutekeleza vyema majukumu yao na kujiepusha na tofauti zinazowafanya washindwe kukabiliana vilivyo na changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu.
Mbinu zinazofaa za kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu zimetakiwa zitumike katika kuleta umoja miongoni mwa Waislamu na kuwafanya wajuane zaidi kiitikadi na kifikra na hivyo kuepuka masuala yasiyokuwa na maana yanayowatenganisha.
Washiriki wa kikao hicho pia wamelaani vikali kitendo cha dharau dhidi ya Uislamu cha kuchanwa na kuchomwa moto Qur'ani Tukufu kilichofanywa hivi karibuni na baadhi ya watu waovu katika nchi za Magharibi na hasa nchini Marekani. Wamesisitiza kwamba kukosewa heshima matukufu ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na maeneo ya ibada na makaburi ya Waislamu ni jambo lisilokubalika kabisa. Taarifa hiyo pia imetaka watu wanaochochea fitina na migawanyiko kati ya Waislamu wachukuliwe hatua za kisheria.
Washiriki pia wametilia mkazo udharura wa kutatuliwa suala la Palestina kwa njia za kiuadilifu na kuwataka Waislamu wote duniani wafanye juhudi za kupunguza machungu ya Wapalestina wanaoteseka chini ya dhulma ya Wazayuni maghasibu. Washiriki pia wamejibari na maghasibu wa Kizayuni na kutaka mzingiro wao wa kidhulma dhidi ya Wapaletina wa Ukanda wa Gaza uondolewe mara moja.
Washiriki wa kikao hicho cha nne cha mjini London wametoa mapendekezo kadhaa ya kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Waislamu ikiwa ni pamoja na kuanzishwa vituo na taasisi maalumu zitakazoshughulikia suala la kuimarisha mazungumzo na fikra ya maelewano miongoni mwa wafuasi wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu. Wamewataka wanazuoni, wanafikra, wasomi pamoja na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu kuchunguza na kufuatilia kwa makini changamoto muhimu zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu na kisha kubuni na kuwasilisha njia za kutatua changamoto hizo.
Wamesema baadhi ya changamoto hizo muhimu ni pamoja na hujuma ya kiutamaduni ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi dhidi ya Waislamu, kupenya magenge ya Kizayuni katika taasisi muhimu za kimataifa za maamuzi, kubuniwa maadui bandia katika jamii ya Waislamu, misimamo ya kisiasa ya nchi za Magharibi dhidi ya maendeleo ya nchi za Kiislamu na kuhodhi kwao teknolojia ya kisasa, kufunika suala la Palestina, kuchochea mivutano ya kimadhehebu, kudhihirisha misimamo ya kupindukia mipaka na finyu kuwa ni ya Kiislamu, kushindwa vyombo vya habari vya Kiislamu kudhihirisha mambo muhimu yanayowakabili Waislamu, udhaifu wa nafasi ya wanawake katika nchi nyingi za Kiislamu na udhaifu wa mawasiliano kati ya jumuiya na taasisi za Kiislamu katika nchi za Magharibi. 668218