IQNA

Baraza Kuu la Misikiti lalaani uchomaji moto Qur'ani huko Palestina

14:18 - October 06, 2010
Habari ID: 2007790
Baraza Kuu la Misikiti linalofungamana na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu limetoa taarifa likilaani vikali uchomaji moto wa Msikiti wa al-Anbiyaa katika kijiji cha Beit Fajjar kilichoko kusini mwa Beit Lahm katika Ukingo wa Mgaharibi wa Mto Jordan.
Katika tukio hilo la jinai, nuskha kadhaa za Qur'ani pia zilichomwa moto na Wazayuni. Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Abdallah Abdul Muhsin at-Turki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu, amesema kuwa hiyo si mara ya kwanza kwa Wazayuni kuvamia na kushambulia misikiti ya Wapalesina bali huko nyuma pia Mayahudi wenye misimamo ya kupindukia walivamia na kuteketeza misikiti mingi ya Waislamu katika ardhi za Palestina ikiwemo ya al-Aqswa na Ibrahim al-Khalil.
Taarifa hiyo imesema kuwa misikiti ni nyumba za Mwenyezi Mungu na kwamba kukosewa heshima nyumba hizo ni kukosea heshima matukufu na vitabu vya Mwenyezi Mungu ikiwemo Qur'ani Tukufu.
At-Turki ameashiria katika taarifa hiyo athari mbaya na hatari za hatua ya Mayahudi walio na misimamo ya kupindukia mipika ya kuchoma moto misikiti na Qur'ani Tukufu na kusisitiza kwamba, jambo hilo ni dharau na udhalilishaji wa wazi kwa Waislamu wote duniani.
Amezitaka taasisi muhimu za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa na Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la umoja huo UNESCO kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kukabiliana na walowezi wa Kiyahudi wanaoyafanyia dharau matukufu ya Kiislamu. Amesema kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya dharau hiyo kitawashajiisha maadui wa Uislamu kuendelea na jinai zao dhidi ya matukufu ya kidini.
At-Turki amesema mwishoni mwa taarifa hiyo kwamba kutetea na kuunga mkono matukufu ya Kiislamu ni jukumu la kila Muislamu na kuzitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC kufanya juhudi za kuzishawishi taasisi muhimu za kimataifa zichukue hatua za kukabiliana na hujuma ya walowezi wa Kizayuni na Kiyahudi wanaoendesha hujuma dhidi ya matukufu ya kidini. 669147
captcha