IQNA

Tasisi ya kimataifa ya kumtetea Mtume (saw) kuasisiwa

14:22 - October 06, 2010
Habari ID: 2007796
Washiriki wa kikao cha kimataifa cha Mtume wa Rehema (saw) nchini Saudi Arabia wametaka kuanzishwa taasisi ya kimataifa ya Kiislamu ya kumtetea Mtume Mtukufu (saw) pamoja na suna zake.
Kwa mujibu wa tovuti ya Tasbih, washiriki wa kikao hicho wamesisitiza kwamba kubuniwa kwa taasisi hiyo kutasaidia kuunganisha taasisi za Kiislamu katika kutetea utukufu wa Mtume (saw) ulimwenguni na pia kuimarisha juhudi za kubadilishana uzoefu katika uwanja huo.
Kikao hicho pia kimesisitiza udharura wa kuchapisha vitabu na majarida na kuanzisha tovuti na televisheni za kimataifa za satalaiti zitakazowafahamisha walimwengu sira, maisha na suna za Mtume (saw) kwa lugha mbalimbali.
Kufuatilia upotofu unaoenezwa duniani kuhusiana na suna za Mtume (saw) na kuujibu kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu pamoja na kuwaunga mkono watafiti wa Kiislamu na kuwasaidia kushiriki katika mikutano ya kimataifa na kutoa hutuba katika vyuo vikuu vya kimataifa kwa lengo la kusahihisha mitazamo mibaya kuhusiana na Mtume (saw), ni miongoni mwa masuala yaliyosisitizwa kwenye taarifa ya mwisho ya kikao hicho.
Washiriki wa kikao hicho pia wametaka kubuniwa sheria za kimataifa za kuzuia kukosewa heshima matukufu ya Kiislamu.
Kikao hicho cha wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu kilifanyika Jumapili na Jumatatu mjini Riyadh, Saudi Arabia. 669394
captcha