IQNA

Qura'ni Tukufu yakosewa heshima mara hii nchini Algeria

13:22 - October 09, 2010
Habari ID: 2009065
Katika hali ambayo radiamali ya kukosewa heshima Qur'ani Tukufu nchini Marekani bado inaendelea kutolewa katika pembe mbalimbali za dunia, mara hii kitendo cha kundi moja lisilojulikana vyema, cha kuchana kitabu hicho kitakatifu nchini Algeria kimeamsha hasira ya wananchi wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la nchi hiyo la al-Shurouq, kundi lisilojulikana katika mji wa Aulad Meimun katika mkoa wa Tlemcen limechana Qur'ani Tukufu na kuiacha mfano wa msalaba na kisha kutupa kurasa zake zilizochanwa mbele ya msikiti mmoja katika mji huo.
Kitendo hicho kimewakasirisha sana wakazi Waislamu wa mji huo ambapo imamu wa msikiti wa Aulad Meimun amevitaka vyombo husika katika mji huo kufuatilia na kuchunguza kwa kina kitendo hicho cha dharau dhidi ya matukufu ya kidini.
Wanazuoni na maimamu wa mji huo wamesema kuwa kitendo hicho kimelenga kuzusha fitina nchini Algeria na kusisitiza kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa kitendo hicho huenda kimefanywa na makundi ya wahubiri wa Kikristo kwa lengo la kueneza dini yao nchini humo. Wanazuoni na maimamu hao wamesema kuwa dharau hiyo inapingana wazi na juhudi za kuimarisha maelewano na uhuru wa itikadi na fikra kati ya wafuasi wa dini tofauti na kuongeza kuwa jambo hilo linabainisha wazi kwamba maadui wa Uislamu hawazingatii thamani wala misingi yoyote ya kiutu. 670466
captcha