IQNA

Ayatullah Khamenei:

Hali ya sasa ya ulimwengu wa Kiislamu ni kama ile ya vita vya Ahzab

11:14 - October 10, 2010
Habari ID: 2009749
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa makundi mbalimbali yanayopinga Uislamu, haki na masuala ya kiroho yamesimama mkabala wa dini tukufu ya Kiislamu na akasema: "Hali ya sasa ni mfano wa vita vya Ahzab na umoja na adhama ya umma wa Kiislamu katika hija inaweza kusambaratisha moyo wa kambi ya maadui wa Uislamu."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo katika mkutano wa maafisa wanaosimamia msafara wa hija wa Iran akisisitiza kuwa mwenendo wa mahujaji wa Iran unapaswa kudhihirisha sifa na wajibu wa mtu binafsi, wa kiroho, kiibada, kijamii na kisiasa wa ibada adhimu na yenye fahari kubwa ya hija.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hija sahihi na kamili ni chemchemi inayotiririka kwa ajili ya kuufaidisha umma wa Kiislamu. Ameongeza kuwa kwa kutilia maanani matatizo na machungu ya ndani ya umma wa Kiislamu na pia hali halisi ya jamii ya kimataifa, kufanyika ibada sahihi na kamili ya hija ni jambo muhimu na dharura zaidi katika kipindi cha sasa kuliko wakati wowote mwingine.
Ameashiria njama za siku zote za maadui wa Uislamu za kuzusha hisia za uduni na kukata tamaa ndani ya mataifa ya Kiislamu na akaongeza kuwa harakati kubwa, ya pamoja, sahihi na ya kuwajibika ya umma wa Kiislamu katika ibada ya hija inaweza kuurejeshea ulimwengu wa Kiislamu hisia za utukufu, nguvu na matumaini.
Ayatullah Khamenei ameashiria suala la kusimama safu moja makundi mbalimbali yanayopinga Uislamu na hakika mkabala wa dini tukufu ya Kiislamu na akasema: "Hali ya sasa ni mfano wa vita vya Ahzab na umoja na adhama ya umma wa Kiislamu katika hija inaweza kusambaratisha moyo wa kambi ya maadui wa Uislamu."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia juhudi za siku zote na mipango inayofanywa na mabeberu kwa ajili ya kupata udhaifu na upenyo wa kuingilia katika ulimwengu wa Kiislamu na akasema maadui wanafuatilia kwa makini mno mipango yao ya kukuza hitilafu ndogo ndogo za umma wa Kiislamu lakini ibada ya hija ambayo inawaunganisha pamoja Waislamu, itazima njama hizo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa umoja ndio haja kubwa zaidi ya ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa vibaraka wa Wazayuni na Marekani wameketi mawindoni kwa shabaha ya kuzusha hitilafu na mifarakano kati ya Waislamu kwa kutumia visingizio mbalimbali vya kimadhehebu, kikaumu, chuki za kikabila na kadhalika wakati wowote Waislamu wanapokurubiana.
Amesema kuwa kutangazwa waziwazi uadui na uhasama wa vyombo vya ubeberu dhidi ya Uislamu kunapaswa kuwa tahadhari na kengele ya hatari kwa dunia ya Kiislamu. Ameongeza kuwa mataifa na nchi za Kiislamu zinalazimika kuwa macho na kuchunga ushetani na hila za kuwatenganisha za maadui, la sivyo Uislamu utapatwa na dhuruba na pigo la adui beberu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa miongoni mwa mbinu za maadui wa umma wa Kiislamu kwa ajili ya kuzusha hitilafu na mifarakano katika umma ni kuimarisha makundi na mirengo iliyopotoka kama Qaramita na Manasibi (wanaowafanyia uadui Ahlul Bait wa Mtume saw) kati ya madhehebu za Shia na Suni. Amesisitizsa kuwa mataifa na serikali za nchi za Kiislamu zinapaswa kutambua haja kubwa ya dunia ya Kiislamu ya kuwepo maelewano, mshikamano na ushirikiano na kushikamana na sababu za umoja.
Akifafanua fursa nzuri ya ibada ya hija kwa ajili ya mazungumzo na maelewano kuhusu masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu ikiwa ni pamoja na kadhia ya Palestina, Ayatullah Khamenei amesema Uzayuni kama chama cha kisiasa kinachochukiwa na hata Wayahudi, unakalia kwa mabavu ardhi za Kiislamu za Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu kwa kipindi cha miaka 60 sasa na kila siku unatenda jinai huku nchi za Waislamu zikinyamaza kimya mbele ya kilio na sauti za kuomba msaada za Waislamu wa Palestina. Amesema harakati adhimu ya hija inaweza kuwa na taathira kubwa katika kuchunguza sababu za kimya na hitilafu hizo na kuanzisha uungaji mkono na himaya ya Waislamu wote kwa taifa la Palestina.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amekosoa mbinyo na mashinikizo wanayowekewa mahujaji wa Iran huko Makka na Madina na akasema kuwa upande huu pia kuna baadhi ya watu wanaojibu mashinikizo na mbinyo huo kwa kuchukua hatua zisizokuwa sahihi. Amesisitiza kuwa mashinikizo na majibu hayo yanapingana na falsafa ya ibada ya hija.
Amesema kuwa hija ya mahujaji wa Kiirani imekuwa na matunda na kukamilika zaidi ikilinganishwa na miaka 30 iliyopita lakini mabadiliko hayo hayatoshi. Amesisitiza kuwa mwenendo wa kila hujaji wa Kiirani unapaswa kuakisi mwenendo sahihi wa mtu binafsi, wa kiibada, kijamii na kisiasa wa ibada ya hija na kuwa dhihirisho la mshikamano na umoja wa umma wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa Waislamu kote duniani kuwasaidia watu waliopatwa na masaibu ya mafuriko nchini Pakistan na akasema kuwa wananchi na serikali ya Iran imetoa misaada kwa jirani zetu wa Pakistan na Mwenyezi Mungu atawalipa mema kwa amali hiyo lakini misaada hiyo haitoshi. Amewataka mahujaji wa Kiirani kupunguza matumizi yasiyokuwa ya dharura katika safari ya hija kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zao walioathiriwa na mafuriko nchini Pakistan na kuwalingania kwa maneno na vitendo mahujaji kutoka nchi nyingine ili wawasaidie Waislamu hao waliopatwa na masaibu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza ratiba na mipango ya taasisi zinazoshughulikia masuala ya hija hapa nchini na amewataka viongozi husika kufuatilia kwa makini utekelezaji wa ratiba na mipango hiyo. 671726

captcha