Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limebainisha wasiwasi wake kuhusiana na hali ya Mashia nchini Bahrain na kutiwa nguvuni kwa wanaharakati 250 wa Kishia katika kipindi ambacho uchaguzi wa bunge unakaribia kufanyika nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo siku ya Jumatatu, imesema kuwa wanaharakati 250 wa Kishia wanazuiliwa na kuteswa katika jela za Bahrain katika hali ambayo uchaguzi wa bunge umepangwa kufanyika nchini Jumamosi tarehe 23 Oktoba.
Wakati huohuo, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limewataka viongozi wa Bahrain wawaruhusu watetezi wa haki za binadamu wa nchi hiyo wasafiri katika nchi nyingine. Viongozi na maafisa wa usalama wa Bahrain wanawashikilia wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu wa Kishia na kuwazuia kusafiri katika nchi za kigeni.
Katika upande wa pili, Chama cha Umoja wa Kitaifa cha Kiislamu cha Bahrain, ambacho ni chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini humo kimetangaza kwamba kitashiriki katika uchaguzi huo wa bunge. 673854