Heinz-Joachim Fischer mwandishi wa Kijerumani ambaye ni mtafiti wa Kikristo ameandika kitabu juu ya uhusiano wa Uislamu na Ukkristo katika zama zilizopita na za sasa, kitabu ambacho amekipa anwani ya 'Baina ya Roma na Makka, Mapapa na Uislamu.'
Kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha ya Kijerumani kimetarjumiwa katika lugha ya Kiarabu na wataalamu wa lugha mbili hizo wa Jumuiya ya Utamaduni na Turathi ya Abu Dhabi.
Kitabu hicho kinazungumzia kwa kina siasa za Vatican kuhusu Uislamu katika karne za 20 na 21 ambapo mwandishi amejaribu kuzingatia zaidi thamani za pamoja za dini mbili hizo, za kuheshimiana wanadamu na udharura wa kujiweka mbali na vitendo vya utumiaji mabavu na misimamo ya kupindukia mipaka.
Kitabu hicho ni muhimu kutokana na ukweli kwamba mwandishi wake amekuwa na uhusiano wa karibu na Vatican pamoja na viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo ya kidini kwa kipindi cha karibu miaka 20. Aliandamana na papa wa zamani wa Vatican aliyemtangulia wa hivi sasa katika safari zake zote katika nchi za Kiislamu, na msomaji wa kitabu hicho bila shaka atapata ufahamu wa kihistoria wa uhusiao wa Uislamu na Vatican katika karne zilizotajwa.
Heinz-Joachim anaashiria katika kitabu hicho misimamo ya mapapa wa hivi karibuni kuhusiana na Uislamu na pia uamuzi wa Baraza Kuu la Vatican kati ya miaka 1962 hadi 1965, wa kushirikiana na kufanya mazungumzo na Waislamu. 673454