IQNA

Kuheshimiwa Wakriso katika Mashariki ya Kati ni jukumu la Kiislamu

11:12 - October 16, 2010
Habari ID: 2013290
Muhammad Sammak, Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo ya Lebanon amesema kuwa kuheshimiwa Wakristo wanaoishi katika Mashariki ya Kati ni jukumu la Kiislamu na kisheria.
Muhammad Sammak aliyekuwa akizungumza huko Vatican katika Baraza la Makanisa ya Mashariki ya Kati, ameongeza kuwa Wakristo wanaoishi katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni wanapambana bega kwa bega na Waislamu dhidi ya maghasibu hao kwa lengo la kutetea haki na ardhi zao, na hivyo kuna udharura mkubwa wa kuheshimiwa Wakristo hao kwa shabaha ya kufikia malengo ya pamoja.
Amesema kwa miaka mingi sasa Wakristo wamekuwa wakiishi kwa amani pembeni ya Waislamu katika Mashariki ya Kati bila kuwepo matatizo yoyote makubwa.
Sammak ambaye pia ni mshauri wa kisiasa wa mufti wa Lebanon amesema katika sehemu nyingine ya hutuba yake kwamba, kuishi pamoja kwa amani Wakristo na Waislamu wa Mashariki ya Kati ni jambo linalobainisha wazi kwamba kuna udharura mkubwa wa wafuasi wa dini mbili hizi muhimu zilizotokana na Nabii Ibrahim (as) kuendelea kuishi pamoja kwa amani. Amesema Waislamu wanapasa kulichukulia suala la kuheshimiwa Wakristo kuwa wadhifa wao wa kidini na kisheria na kudumisha mazungumzo kati yao kwa lengo la kuimarisha amani duniani.
Kikao cha baraza hilo la makanisa kilimalizika jana Ijumaa.
Lengo la kuandaliwa kikao hicho kilichowashirikisha viongozi wa Kikristo na wanafikra kadhaa wa Kiislamu ni kuchunguza hali ya Wakristo wanaoishi katika nchi za Mashariki ya Kati na kutafuta njia za kuimarisha mazungumzo baina yao na Waislamu. 675257
captcha