IQNA

Sheikh wa al Azhar apinga kukufurishwa Waislamu wa Kishia

11:33 - October 16, 2010
Habari ID: 2013386
Sheikh wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri amepinga hatua ya baadhi ya kanali za televisheni za satalaiti ya kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia akisema kuwa hitilafu kati ya Shia na Suni zinazushwa kwa lengo la kutumiwa katika masuala ya kisiasa.
Sheikh Ahmad al Tayyib ameliambia gazeti la al Nahar la Lebanon kwamba hakuna hoja yoyote ya Qur’ani Tukufu au hadithi ya Mtume inayohalalisha kuwakufurisha Mashia.
Amesema kuwa lengo la kuwakufurisha Mashia ni kutaka kuzusha hitilafu kati ya Waislamu wa madhehebu za Suni na Shia na kuzitumia kisiasa hitilafu hizo kama ilivyokuwa kati ya wafuasi wa madhehebu nne za kifiqhi za Suni.
Sheikh wa al Azhar ameongeza kuwa hitilafu zote za Suni na Shia ziko katika suala la uimamu na kusema: “Sisi Masuni tunaswali nyuma ya Shia katika swala za jamaa na tofauti na uvumi unaoenezwa, Shia hawana Qur’ani nyingine ghairi ya hii inayotumiwa na wafuasi wa madhehebu nyingine za Kiislamu.”
Sheikh Ahmad al Tayyib amesema kuwa wajibu wa Chuo Kikuu cha al Azhar katika awamu ya kwanza ni kuimarisha umoja wa Kiislamu na kuwakutanisha Waislamu wote katika mtazamo mmoja licha ya kuwepo hitilafu za kimitazamo na kiijtihadi. Amesema kuwa yuko tayari kwenda kokote kuliko na Waislamu na kwamba iwapo atatembelea Iraq atazuru mji mtakatifu wa Najaf. Amesema kuwa anatarajia kuwa safari hiyo itafanyika baada ya kutatuliwa mgogoro wa kuunda serikali mpya nchini Iraq.
Sheikh Mkuu wa al Azhar amesema kuwa Qur’ani Tukufu inazitambua rasmi hitilafu za watu katika lugha, mbari na itikadi na inazitaja kuwa ni katika suna na taratibu za maumbile ya duniani hii. 675570

captcha