Mkenya Ali Njoroge ambaye ni msanifu katika Kundi la Kimataifa la Kiislamu la Grafiki amesema katika mahojiano na IQNA kuwa, ‘itakuwa bora katika maonyesho ya siku za usoni wawakilishi wa vyombo mashuhuri vya habari katika ulimwengu wa Kiislamu washiriki katika kitengo cha kimataifa cha maonyesho hayo’. Ameongeza kuwa kitengo cha ndani ya Iran katika Maonyesho ya Kimataifa ya Vyombo vya Habari vya Dijitali kilikuwa na bidhaa za kiwango cha juu.
Ali Njoroge ameashiria chuki dhidi ya Uislamu katika baadhi ya nchi za Ulaya na kusema, ‘katika hali ya sasa kuna haja ya kuongeza shughuli za vyombo vya habari vya dijitali ili kuuariifisha Uislamu halisi’.
Kuhusu harakati za vyombo vya habari vya Kiislamu nchini Kenya, Njoroge amesema kuwa, kwa kuzingatia kuwa aghalabu ya watu wa Kenya ni Wakristo, hakuna vyombo vingi vya habari vya Kiislamu nchini Kenya isipokuwa redio chache za Kiislamu.
Kundi la Kimataifa la Kiislamu la Grafiki hujishughulisha na usanifu wa tovuti za Kiislamu kwa lugha mbalimbali, usanifu programu za kompyuta, majarida ya elektroniki, utangazaji wa dini n.k.
Kundi hilo lina wanachama katika nchi kama vile Kenya, Uingereza, Pakistan, India na Lebanon.
676102