IQNA

Jumuiya ya Nchi za Kiislamu yalaani kuenea chuki dhidi ya Uislamu

15:55 - October 18, 2010
Habari ID: 2014945
Kikao cha tisa cha Kamati ya Habari na Masuala ya Utamaduni ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC kimekemea na kulaani vikali kuenea kwa hisia zilizo dhidi ya Uislamu duniani.
Kwa mujibu wa tovuti ya jumuiya hiyo, Mawaziri wa Habari na Utamaduni wa nchi wanachama wa OIC wanaokutana katika kamati iliyotajwa huko Dakar mji mkuu wa Senegal wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusiana na vitendo vilivyopangwa kabla dhidi ya matukufu ya Kiislamu pamoja na ubaguzi unaofanywa dhidi ya Waislamu katika nchi za Magharibi na kulaani vikali vitendo hivyo. Washiriki wa kikao hicho watachunguza uchapishaji wa kitabu kinachomkosea heshima Mtume Mtukufu (saw) pamoja na kufuatilia juhudi za kubuniwa sheria za kimataifa za kuwaadhibu watu wanaochochea vitendo kama hivyo vilivyo dhidi ya matukufu ya Kiislamu.
Ekmeleddin Ihsanoglu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC ameashiria katika kikao hicho kinachofanyika chini ya uenyekiti wa Rais Abdoulaye Wade wa Senegal hatari ya kuenea vitendo hivyo dhidi ya usalama na amani ya dunia na kuitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za pamoja kwa ajili ya kupambana na vitendo hivyo. Amesema uhuru wa kujieleza haupaswi kubadilishwa na kuwa dharau dhidi ya matukufu ya kidini na kueneza chuki za kibaguzi dhidi ya jamii nyingine za wanadamu. Amesema uhuru kama huo unapasa kutekelezwa katika misingi inayokubalika kisheria.
Wshiriki wa kikao hicho wametaka sheria na adhabu kali itolewe dhidi ya watu wanaowabagua Waislamu na kueneza chuki dhidi ya jamii nyinginezo duniani. 676448
captcha