IQNA

Fatuwa ya Sheikh wa sasa wa al Azhar ni sawa na ile ya Sheikh Shaltut

16:20 - October 18, 2010
Habari ID: 2015297
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafuasi wa Madhehebu ya Ahlul Baiti nchini Misri Muhammad al Darini amesema kuwa matamshi yaliyotolewa na Sheikh Mkuu wa al Azhar akipinga kuwakufurisha Waislamu wa madhehebu ya Shia yana umuhimu kama ule wa fatuwa iliyotolewa na Sheikh Mkuu wa zamani wa al Azhar marehemu Sheikh Mahmud Shaltut.
Sheikh Shaltut alikuwa maarufu kwa juhudi zake kubwa za kukurubisha pamoja wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu.
Muhammad al Darini amesema kuwa matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Sheikh wa al Azhar akipinga madai yanayotolewa na baadhi ya watu ya kuwakufurisha Mashia ni hatua muhimu katika njia ya kuondoa dhulma inayofanyika dhidi ya wafuasi wa madhehebu ya Ahlul Bait.
Amesema kuwa kwa kutoa fatua hiyo, Sheikh Ahmad al Tayyib amezima fitina na ugaidi na kupambana na wale wote wanaofanya njama za kuvuruga uhusiano wa Iran na Misri na pia uhusiano wa Misri na Iraq.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafuasi wa Madhehebu ya Ahlul Baiti nchini Misri ameongeza kuwa matamshi ya Sheikh Mkuu wa al Azhar yamewafurahisha mno Mashia wa Misri.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Sheikh Mahmud Shaltut alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa Kisuni aliyekuwa amebobea katika elimu za tafsiri ya Qur'ani, fiqhi na fasihi ya Kiarabu. Aliwahi kuwa Sheikh wa al Azhar na alikuwa mstari wa mbele kuimarisha umoja na mshikamano wa Kiislamu. Mwanazuoni huyo maarufu alitoa fatuwa mashuhuri na ya kihistoria akitambua rasmi madhehebu ya Shia Ithnaasharia na kujuzisha kufuata fiqhi ya madhehebu hiyo. 677581

captcha