IQNA

Ayatullah Shahrudi:

Ni haramu kuwakosea heshima wake za Mtume Muhammad (saw)

16:54 - October 18, 2010
Habari ID: 2015335
Ayatullah Mahmoud Hashimi Shahrudi ametoa fatuwa akisema kuwa ni haramu kumkosea heshima Bibi Aisha, mke wa mtukufu Mtume (saw) na shakhsia wengine wanaoheshimiwa na Waislamu wa madhehebu za Suni.
Ayatullah Shahrudi ametoa fatuwa hiyo akijibu swali lililoulizwa na wanafunzi na wawakilishi wa wanazuoni wakubwa nchini Kuwait.
Amesema kuwa kuwakosea heshima wake wa Mtume Mtukufu ni haramu na kitendo hicho ni katika njama za maadui wa Uislamu za kuzusha hitilafu na mifarakano katika umma wa Kiislamu.
Fatuwa hiyo ambayo imetolewa kufuatia matamshi ya Yasir al Habib, msoni wa Kishia wa Kuwait aliyemvunjia heshima Bibi Aisha imesema kuwa, ni makosa makubwa kumkosea heshima mke wa Mtume (saw) na makundi na madhehebu zote za Kiislamu zinadhurika na kitendo kama hicho. Amesema kuwa maulama wote wa Kishia na Kisuni wamelaani kitendo hicho.
Ayatullah Hashimi Shahrudi ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Vyombo vya Sheria nchini Iran pia amewashukuru maulama wa madhehebu mbali ya Kiislamu waliolaani matamshi ya Yasir al Habib na kusema kuwa matamshi hayo ni kengele ya hatari kwa umma wa Kiislamu kuhusu njama zinazofanywa na maadui.
Siku chache zilizopita pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei alitoa fatuwa kujibu swali la viongozi na wanazuoni wa Kishia wa Saudi Arabia akiharamisha kitendo cha kuvunjiwa heshima mke wa Mtume Muhammad (saw). 677486



captcha