Maonyesho ya vitabu vya Kiislamu ambapo zaidi ya anwani 10,000 za vitabu vilivyo na maudhui mbalimbali za kidini, kiutamduni na kijamii zimewasilishwa, yanafanyika katika mji wa Mumbai nchini India.
Maonyesho hayo yanafanyika pambizoni mwa kikao cha nne cha kimataifa cha Uislamu ambacho kinaendelea katika mji huo.
Mbali na vitabu hivyo utafiti wa kielimu wa zaidi ya wanafikra 2500 wa ulimwengu wa Kiislamu katika nyanja mbalimbali za kifikra, kielimu na kiutamaduni pia unaonyeshwa katika maonyesho hayo.
Kamati inayoandaa kikao hicho imesema kuwa kuna cd zaidi ya 1000 zinazohusiana na uarifishwaji wa Uislamu na mafundisho yake ambazo zitagawiwa wageni wanaotembelea maonyesho hayo.
Kamati hiyo imetangaza kwamba kubainishwa ujumbe wa dini ya Kiislamu kwa jamii ya mwanadamu, majibu ya tuhuma zinazoelekezwa kwa Uislamu, kukabiliana na njama dhidi ya Uislamu, kufahamishwa watu thamani za kimaadili, uadilifu, haki za binadamu za Kiislamu na wito kwa wanadamu wazingatie tauhidi ni baadhi ya masuala muhimu yatakayojadiliwa katika kikao hicho.
Kikao cha nne cha kimataifa cha Uislamu kilichoanza tarehe 22 kinawashirikisha wanafikra na wasomi wa Kiislamu kutoka pembe tofauti za duniani na kimepangwa kumalizika tarehe 31 Oktoba. 682768