IQNA

Taasisi ya mafunzo ya Qur'ani ya Hamad bin Khalid kuzinduliwa nchini Qatar

13:20 - October 30, 2010
Habari ID: 2021937
Taasisi ya mafunzo ya Qur'ani ya Hamad bin Khalid itazinduliwa huko Doha mji mkuu wa Qatar mara tu baada ya kumalizika hija ya mwaka huu.
Akizungumzia suala hilo, Abdallah Omar al-Bakri mkuu wa taasisi hiyo amesema kuwa taasisi hiyo itakuwa na sehemu mbili za mafunzo ya Qur'ani kwa ajili ya wanaume na wanawake na kwamba walimu mashuhuri wa Qur'ani watasimamia shughuli za mafunzo hayo. Amesema taasisi hiyo ambayo imejengwa kwa thamani ya riali milioni 18 za Qatar inatazamiwa kutoa kila mwaka kati ya wanafunzi 30 hadi 40 waliohitimu kuhifadhi Qur'ani nzima.
Al-Bakri amesema kutoa huduma kwa ajili ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu, kuimarisha utamaduni wa kuhifadhi Qur'ani nchini Qatar na kuboresha mfungamano wa matabaka mbalimbali ya wananchi wa nchi hiyo na Qur'ani Tukufu ni miongoni mwa malengo ya kuanzishwa taasisi hiyo. Amesema licha ya kutoa mafunzo ya kuhifadhi Qur'ani taasisi hiyo pia itakuwa ikitoa mafunzo ya tajwidi kwa wanafunzi walio na hamu ya kufuatilia mafunzo hayo.
Abdallah Omar al-Bakri amemaliza kwa kusema kuwa watu walio na umri tofauti watakuwa na uhuru wa kushiriki katika masomo ya Qur'ani katika taasisi hiyo. 684482
captcha