IQNA

Kikao cha kimataifa cha 'Usalama wa Chakula katika Nchi za Kiislamu' nchini Sudan

13:22 - October 30, 2010
Habari ID: 2021938
Kikao cha tano cha kimataifa cha usalama wa chakula katika nchi za Kiislamu kilianza siku ya Alkhamisi tarehe 28 Oktoba huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Imarati WAM, kikao hicho cha siku mbili kilichomalizika siku ya Ijumaa kilifanyika kwa ajili ya kuchunguza usalama wa chakula na maendeleo ya kilimo katika nchi za Kiislamu. Wawakilishi wa nchi 28 wanachama wa Umoja wa Nchi za Kiislamu OIC na wa mashirika 10 ya kieneo na kimataifa wameshiriki katika kikao hicho.
Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, Abdu ar-Rahman bin Hamad al-Atiyyah, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Kiarabu, Umoja wa Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu ni baadhi ya washiriki muhimu walioshiriki katika kikao hicho.
Akizungumza katika kikao cha ufunguzi, Rais Hassan al-Bashir wa Sudan alisisitiza juu ya kutafutwa njia za kuimarisha kilimo na usalama wa chakula vijijini na mijini katika fremu ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa kikao hicho kimefanyika kufuatia uamuzi wa kikao cha Makka cha kuweka mkakati wa miaka kumi wa kudhamini usalama wa chakula katika nchi za Kiislamu. Kuchaguliwa Sudan kuwa mwenyeji wa kikao hicho kumetokana na ukweli kwamba nchi hiyo ilichaguliwa kuwa moja ya nchi tatu zilizowekwa katika mstari wa mbele wa kupambana na mgogoro wa chakula duniani katika kikao cha kimataifa kilichofanyika huko Rome mji mkuu wa Italia. 684509
captcha