Jamal Khashfachi, mhariri mkuu wa zamani wa gazeti la al-Watan la Saudi Arabia amesifu misimamo ya Ayatullah Ali Sistani, Marja' wa Kishia wa Iraq, ya kutetea na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.
Mwandishi huyo amesema kuwa misimamo hiyo ya kupinga mivutano na ghasia za kimadhehebu na kimakundi nchini Iraq inabainisha wazi ufahamu wa mambo na heshima aliyo nayo kiongozi huyo wa kidini miongoni mwa Waislamu.
Khashfachi ameongeza kuwa wito wa Ayatullah Sistani wa kuwasihi Mashia wa Iraq wawe na utulivu na subira na kutojibu mashambulio ya magaidi wanaowalenga kwa ajili ya kudumisha vita vya ndani nchini Iraq, umekuwa na athari kubwa katika kuzuia kuenea kwa vita vya kikabila na kimadhehebu nchini humo.
Kamal Khashfachi alifutwa kazi katika gazeti lililotajwa hivi karibuni kutokana na ukosoaji wake dhidi ya makundi ya kichochezi ya Kiwahabi yanayozusha ghasia nchini Iraq na kumpongeza Ayatullah Sistani kwa msimamo wake wa kutetea na kuunga mkono umoja wa Waislamu nchini humo.
Hivi karibuni Khashfachi alitoa pendekezo la kutunukiwa Ayatullah Sistani Tuzo ya Amani ya mwaka huu ya Mfalme Fahd ambayo hutolewa kila mwaka na Saudi Arabia kwa shakhsia mbalimbali duniani. 686339